Benki ya UBA yatoa msaada wa vitabu vya fasihi Kisarawe

Muktasari:

Benki ya UBA Tanzania imetoa msaada wa vitabu vya fasihi katika Shule za Sekondari za Kimani na Makurunge wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani

Dar es Salaam.  Benki ya UBA Tanzania imetoa msaada wa vitabu vya fasihi katika Shule za Sekondari za Kimani na Makurunge wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani.

Vitabu hivyo vilivyotolewa Jumatatu Februari 11, 2019 kupokelewa na mkuu wa shule ya Kimani,  Mika Bareri na na wa shule ya  Makurunge,  Hassan Ruheye.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa vitabu hivyo  Ruheye amesema, “Ni muhimu kutambua mchango wa kampuni binafsi kama benki ya UBA Tanzania kwa juhudi za dhati za kuunga mkononi Serikali yetu katika kuinua sekta ya elimu nchini.”

“UBA na wadau wengine waendelee kutusaidia katika nyanja mbalimbali ili kuendelea kutengeneza mazingira bora kwa wanafunzi kujifunza na kuongeza uelewa.”

Mkurugenzi mwendeshaji wa benki hiyo, Flavia Kiyanga  amesema, “Tunaamini jamii iliyoelimika inajengwa kutoka katika shule zenye vifaa vya kufundishia vya kutosha hasa vitabu.”

“Ili kuwa na maendeleo endelevu ni muhimu kuwekeza kwenye elimu na leo tunathibitisha dhamira yetu kwa kutoa msaada wa vitabu kwa shule hizi.”

Ofisa elimu wa wilaya hiyo, Patrick Gwivaha amesema msaada huo umekuja wakati muafaka kwa maelezo kuwa shule nyingi zimekuwa na upungufu wa vitabu, akitaka vitunzwe na kutumika ipasavyo.