Benki za biashara zinabadilisha noti chakavu

Muktasari:

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeagiza ubadilishaji wa noti chakavu ufanywe kwenye matawi ya benki za biashara.


Kigoma. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi wenye noti chakavu au zilizoharibika kuzipeleka kwenye matawi ya benki za biashara ili zibadilishwe.

Hayo yamesemwa na meneja msaidizi wa utunzaji fedha na alama za usalama wa BoT, Abdul Dollah alipokuwa akizungumza na wakazi wa Kigoma Mjini leo, Alhamisi ya Machi 7, 2019.

Amewataka benki za biashara zimepewa jukumu la kubadilisha fedha chakavu kutoka kwa wananchi kisha kuzipeleka BoT ili ziteketezwe.

"Benki zote sasa zinapokea fedha mbovu na chakavu na utabadilishiwa kwa kupewa fedha nzima bila kukatwa lengo ni kupunguza usumbufu unaojitokeza kwa wananchi," amesema Dollah.

Amewataka kuacha tabia ya kuuza noti mbovu au chakavu kwa watu wanaozinunua kwa gharama ndogo kwani hata wao huzipeleka kwenye benki za biashara kuzibadilisha kwa thamani halisi.

Licha ya hofu kutoka kwa baadhi ya watu waliodai benki hukataa kubadilisha fedha chakavu, Dollah amesisitiza kwamba BoT imetoa maelekezo kwa benki zote kubadilisha noti hizo.

Kwa upande wake, meya wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, Hussein Ruhava ameitaka BoT kuanza ujenzi wa tawi lake mjini hapa kwani tayari manispaa imetoa kiwanja jirani na ilipo ofisi ya mkuu wa mkoa katika eneo la Mnarani.

Mfanya biashara katika Soko la Kigoma, Mathias John ameiambia MCL Digital kwamba mpango wa kubadilisha noti chakavu utasaidia kupunguza fedha mbovu zilizopo kwenye mzunguko.

Amewaasa wenye mazoea ya kuchafua noti kutokana na shughuli zao kuwa makini kwani Serikali inapata hasara kuteketeza noti mbovu na kutengeneza mpya.

Wananchi wa Kigoma Mjini wanaweza kubadilisha fedha chakavu katika matawi ya benki ya CRDB, NMB, NBC, TPB na Exim yaliyopo mpaka sasa.