Benki zatakiwa kutumia fursa kufungwa maduka ya kubadilishia fedha

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amezitaka Benki mkoani humo kutumia vizuri fursa ya kufungwa maduka ya kubadilisha fedha kufanya kazi saa ishirini na nne.


Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amezitaka Benki kufanya kazi saa ishirini na nne ili kutumia vizuri fursa ya kufungwa maduka ya kubadilisha fedha mkoani humo.

Maduka zaidi ya 30 ya kubadilisha fedha katika jiji la Arusha yalifungwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tangu Oktoba 2018, kwa kile kilichoelezwa kukiuka taratibu za biashara.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 14, 2019 wakati akifungua semina ya wafanyabiashara na wajasiriamali wa Mkoa huo iliyoandaliwa na Benki ya CRDB, Gambo amesema tangu kufungwa kwa maduka ya kubadilisha fedha kumekuwa na changamoto kwa watalii kubadilisha fedha.

Amesema benki ya CRDB ni moja ya benki kubwa nchini inayoweza kusaidia kuondoa changamoto hiyo.

“Nakuomba mkurugenzi ukipata fursa kakutane na chama cha mawakala wa utalii (Tato) wakueleze changamoto zao na uone utasaidia vipi,” amesema.

Kwa upande wake mkurugenzi mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema benki hiyo tayari imefungua dirisha maalum la kubadilisha fedha katika matawi yake yote, likiwemo lilipo Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro (Kia).