Boeing, FAA matatani kuiruhusu MAX 8

Muktasari:

Kampuni hiyop inayotengeneza ndege pamoja na mamlaka inayosimamia usafiri wa anga zinachunguzwa kuhusu utoaji wa kibali cha kuruhusu ndege aina ya 737 MAX 8 kufanya safari za abiria.


Kampuni ya Boeing na mamlaka inayosimamia usafiri wa anga nchini Marekani zimeingia matatizoni kuhusu kutoa kibali kwa ndege aina ya Boeing 737 MAX baada ya kutokea ajali mbili ambazo mazingira yake yanafanana.

Machi 11, siku moja tu baada ya ndege ya Shirika la Ethiopia kuanguka na kuua watu 157, waendesha mashtaka jijini Washington walipeleka hati ya kuitwa shaurini kwa angalau mtu mmoja aliyehusika katika kutoa kibali cha ndege za aina hiyo, kwa mujibu wa jarida la Wall Street ambalo liliwakariri watu walio karibu na suala hilo.

Wito huo, ambayo ilitoka kwa mwendesha mashtaka katika divisheni ya jinai katika Wizara ya Sheria, unataka nyaraka na mawasiliano yanayohusu ndege hiyo, kwa mujibu wa ripoti hiyo.

Uchunguzi huo wa jinai ni hatua mpya, alisema Scott Hamilton, mkurugenzi mkuu wa kampuni ya Leeham, ambaye alikumbusha uchunguzi uliofanywa mwaka 1996 kuhusu ajali ya ndege ya ValuJet.

"Tofauti na Ufaransa, ambako uchunguzi wa jina katika ajali za ndege ni wa kawaida, ni mara chache sana kutokea nchini Marekani," aliongeza Hamilton.

Inspekta jenerali wa Wizara ya Usafirishaji anachunguza jinsi Mamlaka ya Usimamiziw a Anga (FAA) ilivyoidhinisha kwa ndege hiyo, Wall Street imeripoti. Hakuna aliyepatikana kuzungumza na AFP kuhusu suala hilo.

Uchunguzi huo unalenga mfumo wa ndege hiyo unaohusishwa na ajali ya ndege ya Lion Air ambao mamlaka zinasema umeonyesha tabia zinazofanana pia katika ajali ya ndege ya Ethiopia.

Ndege ya Ethiopian Airlines ilipata ajali Machi 10, ikiwa ni kipindi kisichozidi miezi mitano baada ya ndege aina ya 737 MAX 8 iliyokuwa inamilikiwa na Lion Air kuanguka na kuua watu 189.

Wakati itachukua miezi kadhaa kuweza kukamilisha uchuynguzi, viongozi wa Ethiopia wamesema kulikuwa na mambo yanayofanana katika ajali hizo kwa kuangalia taarifa walizopata katika kifaa kinachorekodi taarifa za ndege.