Boeing 737 Max 8 zasimamishwa

Friday March 15 2019

Waokoaji na wachunguzi wa ajali ya ndege ya

Waokoaji na wachunguzi wa ajali ya ndege ya Ethiopian Airlines aina ya Boeing 737 MAX 8 wakiendelea na kazi ya kukusanya mabaki ya ndege hiyo iliyoanguaka katika Kijiji Hama Quntushele nchini Ethiopia. Picha na AFP 

By George Njogopa na mashirika ya habari [email protected]

Dar es Salaam. Wakitumia mtandao wa Twitter jana, maofisa wakuu wa kampuni ya Boeing inayotengeneza ndege za Boeing 737 MAX 8 wameutangazia ulimwengu kusitisha matumizi yake, kufuatia ajali ya ndege ya shirika la Ethiopian Airlines.

Uamuzi wa kampuni hiyo umekuja muda mfupi baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutangaza amri ya dharura ya kusitisha usafiri wa ndege zote za Boeing 737 Max 8 na Max 9 kwenye anga la nchi hiyo.

Trump alisema marufuku hiyo itaendelea hadi pale uchunguzi utakapokamilika kubaini iwapo hitilafu ya kimitambo ilisababisha ajali mbili za ndege aina ya Max 8 katika kipindi cha chini ya miezi mitano na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Mbali na ile ya Ethiopian Airlines iliyotokea Machi 10 na kuua watu 157, ajali nyingine ya ndege hizo ilitokea Oktoba, 2018 nchini Indonesia ikiwa ni mali ya shirika la Lion Air na kuua watu 189.

Kupitia mtandao wa Twitter, maofisa wa Boeing walisema kampuni hiyo inaunga mkono kauli ya rais huyo na kuongeza kwamba “ni heri kuwa salama kuliko kujuta baadaye.”

Hata hivyo, kwa upande wa Marekani hatua ya kusitisha safari za ndege hizo imekuja siku tatu baada ya msimamo wa awali wa Mamlaka ya Safari za Anga Marekani (FAA), ambayo Jumanne ilitangaza kwamba haikuwa na mipango ya kusitisha safari.

Katika amri yake, Trump alizitaka ndege zote za muundo wa Max 8 na Max 9 ambazo zilikuwa angani wakati wa tangazo hilo ziegeshwe punde tu zitakapotua. “Marubani wote wamefahamishwa hilo pamoja na mashirika yote ya ndege,” alisema Trump.

Kufikia Jumapili ambapo ajali ya Ethiopian Airlines iliyokuwa ikielekea mjini Nairobi ilitokea, Boeing ilikuwa imeuza ndege 370 ulimwenguni kote.

Mtihani mzito Boeing

Kwa sasa kampuni ya Boeing inakabiliwa na mtihani mkubwa kibiashara kwa upande wa ndege hizo, pamoja na ule wa kisheria unaoweza kuibuka wakati wowote.

Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, shirika hilo kubwa la uundaji wa ndege na mitambo ya anga za juu huenda likajikuta likifikishwa mahakamani na mashirika mbalimbali ya usafirishaji wa anga duniani ambayo yamesimamisha ndege hizo.

Pia, mtihani wa kushtakiwa unainyemelea Boeing kutoka kwa kampuni zilizokuwa zimelipia na ambazo ziliweka ‘oda’ ya kutengenezewa ndege hizo, hasa iwapo mchakato wa ukamilishaji utachelewa.

Advertisement