Boko Haram wachafua hali ya hewa Nigeria

Muktasari:

Wagombea urais mahasimu nchini humo wamepiga kura na kuamsha shamrashamra za wananchi waliokuwa kwenye vituo vya upigaji kura


Lagos, Nigeria. Mwanajeshi mmoja ameuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika shambulio la kutumia mabomu ya kutupa kwa roketi lnalodaiwa kufanywa na kundi la Boko Haram Kaskazini Mashariki mwa Nigeria.

Tukio hilo limetokea leo hii, saa chache kabla ya kuanza kwa uchaguzi mkuu nchini humo.

Taarifa kutoka nchini humo zilisema kwamba mpiganaji wa kiraia kutoka mji mkuu Maiduguri, jimbo la Borno, aliliambia Shirika la Habari la AFP kwamba milipuko 13 ilisikika katika mji huo saa 12 za asubuhi.

Wakaazi wa eneo hilo pia walithibitisha kusikia milio ya mashambulizi na ofisa mmoja wa usalama alisema magaidi wa Boko Haram walijaribu kuingia katika mji huo lakini waliweza kuzuiwa.

Ofisa mwingine alisema moja ya mashambulizi hayo lililenga makao makuu ya Jeshi la Nigeria wakati wanajeshi wakijitayarisha kwenda kwenye shughuli zao.

Wasiwasi wa kutokea shambulio kubwa la Boko Haram umezidi kuongezeka wakati wa uchaguzi huo, ambao kundi hilo la kigaidi limeapa kuuvuruga.

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari alishapiga kura yake katika uchaguzi huo wa rais unaofanyika leo nchini Nigeria, ambao umecheleweshwa kwa wiki nzima.

Mpinzani mkuu wa Buhari anayegombea muhula wa pili madarakani, katika kinyang'anyiro hicho cha kuliongoza taifa hilo lenye uchumi mkubwa barani Afrika ni Atiku Abubakar.

Atibu ni mfanyabiashara na makamu wa zamani wa rais huku wachambuzi wengi wakidai kwamba wanatarajia mchuano mkali kati ya wagombea hao wawili.

Buhari alipiga kura yake katika mji alikozaliwa wa Daura, jimbo la Kaskazini la Katsina. Na Abubakar alipiga kura yake muda si mrefu huko Yola mji mkuu wa jimbo la Adamawa.

Shirika la habari la Reuters liliripoti kwamba upigaji kura ulianza saa mbili asubuhi, na raia wa Nigeria walionekana kupanga foleni katika vituo vya kupigia kura nchini kote.

 Baadhi ya vituo vilichelewa kufunguliwa. Raia milioni 72.8 wana haki ya kupiga kura nchini humo.