Bosi Mbelgiji wa kampuni ya simu ya MTN atimuliwa Uganda

Muktasari:

Kampuni hiyo ya MTN ambayo ni maarufu barani Afrika inahudumia nchi 22 kutoka ofisi zake za nchini Uganda.


Uganda imemrejesha kwao kiongozi wa kampuni ya simu ya MTN ya Afrika Kusini usiku wa kuamkia leo, huku polisi wakisema alikuwa tishio kwa usalama wa taifa.

Msemaji wa polisi, Fred Enanga alisema ofisa huyo mtendaji mkuu wa MTN Uganda, Wim Vanhelleputte, ambaye ni raia wa Ubelgiji, ametimuliwa kutokana na "masuala ya usalama wa taifa".

"Tayari yuko uwanja wa ndege na anaelekea Ubelgiji usiku," alisema Enanga jana.

Vanhelleputte amekuwa katika nafasi ya CEO tangu Julai 2016 katika tawi la Uganda ambalo linaendesha huduma ya mawasiliano ya simu kwa nchi 22 za Afrika.

Kutimuliwa kwake kumekuja katika kipindi cha karibu mwezi baada ya raia mmoja wa Ufaransa na mfanyakazi Mnyarwanda kulazimishwa kuondoka Uganda kwa madai ya kutumia nafasi zao "kuweka rehani usalama wa taifa".

Julai mwaka jana, MTN ilisema watu wenye silaha waliodai kuwa wanatokea Taasisi ya Usalama wa Ndani, waliwateka wakandarasi wawili na kuwalazimisha kufungua sehemu kuu ya taarifa ya kampuni hiyo na kujaribu bila mafanikio kuzifikia serva.

Wakati huo, MTN Uganda ilisema ilichukulia tukio hilo "la kihalifu" kwa uzito na iliripoti kwa mamlaka, huku ikiongeza kuwa haiamini kwamba iko chini ya uchunguzi.