MUUNGANO WA TANGANYIKA-ZANZIBAR 1964: Bunge la dharura laitwa Dar kwa ajenda maalumu-10

Friday April 19 2019

 

Oscar Kambona, ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, aliwasili Dar es Salaam mchana wa Aprili 19 akitokea Kigoma. Alikutana na uvumi uliokuwa umeenea mjini Dar es Salaam kuwa Sheikh Karume na familia yake yote alikuwa amekimbilia Dar es Salaam kujificha.

Mara moja Kambona alianza kujibu mapigo. “Huo ni uvumi tu,” aliliambia gazeti la The Nationalist and Freedom la Tanu.

Alisema Karume alikuwa Dar es Salaam kwa mazungumzo na Rais Nyerere juu ya “kuimarisha urafiki kati ya nchi mbili hizi”.

“Kwani hamjui kwamba vyama vyetu (Tanu na ASP) vina usemi unaofanana (wa ‘tutaishi pamoja au tutakufa pamoja?’)” alihoji katika habari hiyo.

Siku hiyo baada ya Kambona kutua mjini Dar es Salaam, alikutana na Nyerere na walifanya mazungumzo ambayo hayakuripotiwa na vyombo vya habari. Hapo ndipo Nyerere alipomwambia kile alichomwitia, kwamba lile wazo alilopata la kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar linafaa na sasa lilitakiwa kufanyiwa kazi haraka.

Muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Kambona, mjini Dar es Salaam, Nyerere aliongea na Karume. Haijulikani kama alimweleza kuhusu suala la Tanganyika kuungana na Zanzibar, lakini inawezekana hilo ndilo lililokuwa shabaha ya mazungumzo yao, na pengine hapo ndipo Karume aliposikia pendekezo la kuunganisha nchi zao kwa mara ya kwanza kabisa, lakini Karume hakuwa ameliwazia kabla ya hapo.

Inasemekana Karume alijaribu kupinga wazo hilo, pengine kwa sababu aliona kuwa cheo chake cha ukuu wa nchi kinahatarishwa. Lakini Nyerere alikuwa na njia nyingi za kumshawishi Karume akubaliane naye kuliko Karume alivyokuwa na njia nyingi za kumpinga Mwalimu.

Alivyoona msimamo wa Karume ulivyokuwa mzito juu ya suala hilo, inaelezwa kuwa Nyerere alitumia ushawishi zaidi ikiwa ni pamoja na kumuahidi ulinzi zaidi. Zanzibar kulikuwa na mamia ya polisi wa Tanganyika waliokuwa wakimlinda baada ya mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Ilibidi amuombe nafasi ya kulitafakari jambo hilo na kuwashirikisha maofisa wa serikali yake ambao wangeweza kumwelewa Nyerere. Hapo ndipo ilipombidi aende Zanzibar na kuwatuma maofisa wake kwenda Dar es Salaam kuzungumza na Nyerere.

Karume alirejea Zanzibar jioni hiyo kwa ndege ya serikali. Saa moja baada ya Karume kuwasili, maofisa kadhaa wa serikali ya Zanzibar waliwasili mjini Dar es Salaam. Miongoni mwao alikuwemo Makamu wa Rais wa Zanzibar, Kassim Hanga na Waziri wa Fedha na Maendeleo, Abdul Aziz Twala.

Siku iliyofuata, Mwalimu Nyerere alitoa agizo kwa katibu wa Baraza la Taifa (Bunge) awaite wajumbe kutoka maeneo yote nchini kwa ajili ya kikao cha dharura mjini Dar es Salaam.

Alimwambia Spika wa Bunge, Adam Sapi Mkwawa kuwa “kikao cha dharura kitashughulikia jambo muhimu la manufaa kwa taifa”.

Mwalimu alifanya kazi haraka, mawaziri wakitumwa huku na huko. Dakika, saa, halafu siku, zilikuwa zikipita upesi. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa maandalizi ya Muungano wa Tanganyika-Zanzibar.

Kadiri maandalizi yalivyokuwa yakiendelea, Balozi Leonhart alianza kuwa na kazi nyingi za kutoa taarifa za matukio ya siku kwa siku. Sasa aliona muda ulikuwa ukienda haraka kuliko awali.

Kile ambacho yeye na serikali yake walikuwa wakikisubiri kwa kipindi chote, ndicho kilichokuwa kikikaribia. Siku hiyo pia, Balozi Leonhart alituma ujumbe kwenda Marekani ukisema: “Mradi wa Tanganyika-Zanzibar sasa umefikia hatua muhimu sana.”

Baada ya wazo la kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar kuonekana kuwa limekubalika, Shirika la Kijasusi la Marekani (CIA) lilianza kutafakari njama za kumzuia Abdulrahman Mohamed Babu asirejee Zanzibar.

Kwa kuiona hatari iliyopo, balozi wa Marekani nchini Tanzania, William Leonhart alituma ujumbe Marekani.

“Huenda tukahitaji kufanya kazi haraka bila kukawia. Jaribio lolote la kutaka kumuondoa (Abdulrahman) Babu, (Salim) Rashid na mfuasi yeyote anayewatii watu hawa linaweza pia kuharakisha fujo zitakazolazimisha matumizi ya nguvu kutoka nje ya Zanzibar,” alisema katika telegram hiyo.

Akijibu ujumbe wa simu za maandishi zilizotajwa hapo juu, Naibu Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa Marekani, George Wildman Ball, alisema: “Idara (CIA) inatoa baraka zake zote kwa kuunga mkono hatua zilizochukuliwa na Tanganyika: Shirikisho la Tanganyika-Zanzibar au Muungano.

“Mpaka kufikia hatua hii hatujapata ishara ya kuombwa msaada wowote ambao Marekani inatakiwa kuutoa. Na kama kuna (msaada) wowote unaohitajika, ambao Kambona anaweza kuuomba atakapokuja kukuona tena Aprili 20, ni vizuri tukajulishwa mapema tuweze kuuandaa.”

“Kwa maoni yetu,” anasema George Ball katika majibu yake kwa Balozi Leonhart, “ingefaa sana kama Kambona angekuwa ndiye wa kwanza kutuomba sisi tumpe msaada badala ya sisi kumwambia kwamba tutampatia msaada wowote na akuambie ni aina gani ya msaada anaohitaji ili aendeleze kile kitakachoonekana kana kwamba ni kitendo cha Waafrika wenyewe (cha kuungana) ili isije ikaonekana kwamba Marekani imeshiriki katika mpango huo au kuonekana kama inataka kupindua nchi nyingine.

“Hata hivyo, ikiwa itaonekana kuwa ni faida kwetu kutoa kwa hiari yetu mojawapo ya mambo yafuatayo ili kufanikisha shabaha zetu, unaweza kufanya hivyo: (i) Ipe Marekani baraka kutokana na mpango ulioandaliwa na Kambona wa kupata ushirikiano wa Tanganyika-Zanzibar (Shirikisho la Tanganyika-Zanzibar) ambao hautamjumuisha Babu na kikundi chake (cha watu wenye itikadi za Kikomunisti).

“Pia suala la pili lilikuwa ni kuonyesha “kwamba Serikali ya Marekani ina moyo wa kutoa msaada, hata kama ni wa muda mfupi”, na tatu ni kumthibitishia “Kambona kwamba Serikali ya Marekani iko tayari kutafakari na kuzingatia na kufanya kazi haraka iwezekanavyo juu ya mahitaji ya misaada inayotakiwa”.

Advertisement