Bunge laishauri Serikali ya Tanzania kushirikisha wadau uandaaji wa miswada ya sheria

Muktasari:

  • Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 27, 2019 na Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria katika maoni yake kuhusu muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba tatu wa mwaka 2019 uliowasilishwa bungeni leo.

Dodoma. Kamati ya Bunge la Tanzania ya Katiba na Sheria imebaini changamoto ya ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa uandaaji wa miswada mbalimbali ya sheria  hasa ya dharura.

Hayo yameelezwa leo Alhamisi Juni 27, 2019 na makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Najma Giga wakati akisoma maoni ya kamati hiyo bungeni jijini Dodoma kuhusu muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali namba tatu wa mwaka 2019 uliowasilishwa bungeni leo.

Muswada huo unapendekeza marekebisho katika sheria nane ambazo ni Sheria ya Makampuni (sura ya 212), Sheria ya Hakimiliki (sura ya 218), Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza (sura ya 230), Sheria ya Mashirika yasiyo ya Kiserikali (sura ya 56), Sheria ya Vyama vya Kijamii (Sura ya 337), Sheria ya Takwimu (sura ya 351), Sheria ya Uwakala wa Meli (sura ya 415) na Sheria ya Muunganisho wa Wadhamini (sura ya 318).

Kwa nyakati tofauti wadau mbalimbali zikiwemo asasi za kiraia (NGOs) zimeyalalamikia marekebisho hayo kwa maelezo kuwa yanakwenda kuwabana.

“Maoni ya wadau ni muhimu kwa hatua zote za mchakato wa kutunga sheria zenye tija katika sekta husika, kwa wadau hao ndio wanajua changamoto za sekta husika na namna bora ya kuondoa changamoto hizo.”

“Serikali iendeleze utamaduni wake wa kushirikisha wadau wote wakati wa kuandaa miswada mbalimbali ya sheria kwa lengo la kuliwezesha Bunge kutunga sheria zenye mawazo jumuishi kwa ustawi wa nchi pamoja na kupunguza changamoto zisizo za lazima wakati wa utekelezaji wa sheria hizo miongoni mwa wadau wanaoguswa na sheria hizo,” amesema Giga.

Katika maoni yake kamati hiyo iliunga mkono marekebisho hayo yaliyoletwa na Serikali ya Tanzania, huku baadhi ya maeneo ikipendekeza namna bora zaidi ya kuwekwa ili kuleta mantiki zaidi.

Mfano ibara ya 35 ya sheria ya vyama vya kijamii inayopendekeza muda wa miezi miwili kwa taasisi kuwa zimekamilisha mchakato wa kutekeleza masharti yaliyopendekezwa, kamati hiyo imeshauri kuongezwa ili iwe miezi mitatu ili kuzipa muda taasisi hizo kukamilisha mchakato wa kuhamia katika sheria zinazowahusu.

“Kifungu kitoe mamlaka kwa waziri mwenye dhamana kuongeza muda kwa taasisi itakayowasilisha maombi ya kuongezewa muda pale itakaposhindwa kukamilisha mchakato wa kutekeleza matakwa ya sheria hii ndani ya muda uliopangwa,” amesema Giga.