Busu la Papa Francis huenda likamaliza uhasama Sudan Kusini

Tuesday April 16 2019

 

Haikuwa kazi rahisi kufikia hatua ya kuwa na mamlaka kamili ya kujitawala kwani walilazimika kutumia miaka mingi wakipambana kwa namna mbalimbali ikiwamo kupigana na ndugu zao wa Sudan wakati huo wakiwa ni nchi moja.

Hata hivyo, miaka miwili baada ya nchi hiyo kuwa huru iliingia katika machafuko makubwa na kujikuta katika hali ngumu ya ustawi wake kuliko ilivyotarajiwa.

Mpaka sasa takribani watu 400,000 wanakadiriwa kupoteza maisha kutokana na mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe huku viongozi wake wakuu na wanasiasa wenye sauti kubwa Rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Riek Machar, wakitajwa kuwa ndio wanaoweza kuliweka pamoja taifa hilo.

Kutokana na ukweli huo huo na umuhimu wa amani katika nchi hiyo, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis Aprili 11, mwaka huu aliandaa ibada maalumu na mazungumzo yaliyowashirikisha Kiir, Machar na viongozi wengine waandamizi wa Sudan Kusini.

Wengi wamepongeza uamuzi wa Papa Francis aliyeshirikiana na viongozi wengine wa dini akiwamo kiongozi wa Kanisa Anglikana, Askofu wa Canterbury, Justin Welby aliyehusika pia katika kushauri kuandaliwa kwa jambo hilo.

Papa Francis akizungumza na viongozi hao ambao mwezi ujao wataanza kuendesha Serikali ya pamoja, aliwataka kuhakikisha wanatanguliza amani na maslahi ya nchi yao japo anatambuwa kuwa katika kuendesha Serikali hiyo kunaweza kutokea tofauti za kimitazamo.

Kiongozi huyo mwenye heshima kubwa duniani, kabla ya kuanza mazungumzo na ujumbe wa viongozi hao, licha ya umri wake mkubwa wa miaka 82 na kuwa na tatizo la miguu, lakini kwa msaada wa wasaidizi wake alibusu miguu ya viongozi hao kitendo kinachotafsriwa kubeba ujumbe mzito katika kuhakikisha Sudan Kusini inakuwa na amani.

Alimtaka Kiir, Machar na makamu wa rais watatu wa nchi hiyo kuheshimu makubaliano waliyoingia kuunda Serikali ya umoja itakayoanza kutekelezwa Mei mwaka huu.

“Nakuombeni kama ndugu endeleeni kubaki katika amani. Nakuombeni kwa moyo wangu sasa twende mbele. Kunaweza kujitokeza matatizo mengi lakini hayawezi kutuondoa. Tatueni matatizo yenu,” alisema Papa Francis.

Alisema “kunaweza kutokea kutoelewana miongoni mwenu, lakini tofauti zenu ziishie kwenu viongozi, katika ofisi zenu. Mbele ya watu wengine shikaneni mikono. Mkifanya hivyo mtakuwa mababa wa taifa”.

Pande mbili zinazoongozwa na Kiir na Machar, Septemba mwaka jana zilitia saini makubaliano ikiwa ni kuelekea katika kuunda Serikali ya pamoja kama njia ya kumaliza mgogoro unaonasibishwa na ukabila baina ya Dinka na Nuer na kuwania madaraka.

Papa Francis katika ujumbe wake alisema Wasudan Kusini wameumizwa sana na vita na kwamba viongozi wanalo jukumu la kuijenga nchi yao changa katika misingi ya haki.

“Sitachoka kurudia kusema kuwa amani inawezekana. Ni zawadi kubwa ya Mungu lakini pia ni jukumu muhimu zaidi kwa wenye mamlaka ya kuwaongoza watu. Sote tunapaswa kuwa wasaka amani. Jengeni amani kwa njia ya mazungumzo, masikilizano na kusameheana. Kumbukeni kuwa vita hupoteza kila kitu,” alisema.

Papa Francis alihitimisha mazungumzo yake na viongozi kwa sara ambapo alimuomba Mungu kugusa nyoyo za wote wanaohusika ili kutanguliza amani, umoja na upendo.

Athari za mgogoro huo

Moja ya athari za mgogoro huo uliosababisha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe tangu ulipoibuka mwaka 2013 ni njaa kwa Wasudan Kusini.

Inaelezwa kuwa bei ya vyakula nchini humo imepanda kwa asilimia 70 huku takribani watu milioni 6.3 wakielezwa kutokuwa na uhakika wa chakula kwa kila siku kwa takwimu zilizotolewa mwanzoni mwa mwaka 2018.

Masoko mengi ya vyakula yamefungwa na asilimia kubwa ya wakulima wameyakimbia maeneo yao.

Awali mwaka 2017 taifa hilo ambalo ni moja ya nchi sita zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lilitangazwa kuwa katika hali mbaya ya chakula huku juhudi za mashirika ya kimataifa kufikisha misaada zikikumbana na kikwazo cha mapigano.

Licha ya kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano na kuunda Serikali ya pamoja kama yale yaliyofikiwa mwaka 2015, bado hakujashuhududiwa utulivu wa kweli unaotoa fursa kwa nchi hiyo changa kujikita katika kupiga hatua mbalimbali za kimaendeleo.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), unahitajika msaada mkubwa zaidi kwa ajili ya kusaidia familia zilizoathirika na mgogoro huo hasa kwa upande wa afya. Inaelezwa kuwa kutokana na idadi kubwa ya watu kuyakimbia makazi yao, miundombinu mbalimbali hasa ya kielimu na afya nayo imeathirika.

Advertisement