CAG aanika sababu za kukatikatika kwa umeme

Muktasari:

  • Kwa mujibu ripoti hiyo inaonyesha usimamizi mbovu wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya matengenezo ya mitambo, kutokuwa na mipango ya ununuzi wa vipuri unaosababisha bei kuwa kubwa zaidi ya iliyo kwenye bajeti, kutofuatwa kwa mfumo wa manunuzi katika baadhi ya vituo na kutofanyika kwa utafiti wa bei ya vipuri kabla ya kwenda kununua.

Dar es Salaam. Matengenezo yenye ufanisi na yanayofaa ya mitambo ya kufua umeme ni muhimu katika kuhakikisha kunakuwepo na umeme wa uhakika, lakini ripoti ya ukaguzi wa ufanisi katika utendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco) inaonyesha hali tofauti.

Ripoti imebainisha udhaifu katika maeneo mengi unaosababisha umeme kutokuwa wa uhakika na kukatika mara kwa mara kwa nishati hiyo muhimu.

Ripoti hiyo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ambayo imeangalia utendaji wa Tanesco kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2015/16 ni moja kati ya ripoti kadhaa za ukaguzi wa utendaji wa taasisi za Serikali zilizowasilishwa bungeni mwezi huu pamoja na ripoti za ukaguzi wa fedha za Serikali Kuu na taasisi zake.

Alipoulizwa kuhusu hatua zilizochukuliwa katika utekelezaji wa mapendekezo ya ripoti za CAG, mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na msemaji mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi alisema Serikali itawasilisha utekezaji wa ripoti yote ya CAG bungeni na kwenye Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) mjadala utakapoanza.

“Ila mengi yameshafanyiwa kazi kwa sababu hiyo ripoti ni ukaguzi wa nyuma sana. Takribani miaka miwili iliyopita,” alisema katika majibu yake aliyotuma kwa ujumbe wa maandishi kwa simu, juzi.

Kwa mujibu ripoti hiyo inaonyesha usimamizi mbovu wa ununuzi wa vipuri kwa ajili ya matengenezo ya mitambo, kutokuwa na mipango ya ununuzi wa vipuri unaosababisha bei kuwa kubwa zaidi ya iliyo kwenye bajeti, kutofuatwa kwa mfumo wa manunuzi katika baadhi ya vituo na kutofanyika kwa utafiti wa bei ya vipuri kabla ya kwenda kununua.

Ripoti hiyo pia imesema tatizo jingine ni zabuni mbalimbali kutotekelezwa kutokana na kutokuwepo kwa fedha za kutosha, wafanyakazi wenye stadi maalumu katika mitambo ya uzalishaji umeme kutotosha, kutofanyika kikamilifu kwa utafiti kujua mahitaji ya mafunzo ya wafanyakazi na kusababisha utafiti huo kuhusisha asilimia 36 tu ya wafanyakazi

Vilevile, kutofanya uchunguzi kwa ajili ya kutambua maeneo yanayoweza kusababisha athari na hivyo kusababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara na kutofanyika kwa uchambuzi kujua mwelekeo wa matatizo na historia ya mitambo na vipuri.

Pia, taarifa hiyo imebaini kuwa Tanesco haijaweka kipaumbele cha athari kwa ajili ya kuchukua hatua za kuzuia, kutoweka kipaumbele katika kutumia malengo yaliyokusudiwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya matengenezo na kusababisha kutotengenezwa kwa mitambo ambayo ilitakiwa ifanyiwe matengenezo makubwa na kutokuwepo kwa mfumo wa utoaji taarifa za matengenezo kwa Wizara ya Nishati.

Hali kadhalika, ripoti hiyo imesema Tanesco haisimamii kikamilifu matengenezo ya mitambo ya kufua umeme, haina mfumo fanisi wa kusimamia matengenezo ya mitambo, huku Wizara ya Nishati ikionekana haina usimamizi fanisi wa mitambo ya kufua umeme.

“Tanesco haikufanya kikamilifu matengenezo yanayozingatia athari zilizopo katika mitambo ya ufuaji umeme kwa ajili ya kuhakikisha kupatikana kwa umeme wa uhakika na kuwa na uwezo wa kutosha wa ugavi wa umeme kwa mwaka mzima,” anasema CAG katika majumuisho ya muhtasari wa ripoti hiyo.

Katika suala la kukatika kwa umeme mara kwa mara, ripoti hiyo inasema Novemba, 2017 mikoa yote nchini ambayo imeunganishwa katika gridi ya Taifa ilikosa umeme kutokana na matatizo ya kiufundi. Pia inaeleza jinsi taarifa za kukatika mara kwa mara kwa umeme ambao unatokana na maji, gesi asilia na mafuta mazito.

“Athari hizi za kukatika kwa umeme kumeathiri uwekezaji katika viwanda na biashara,” anasema CAG katika taarifa hiyo iliyoandaliwa na Injinia Andrew Kellei, aliyeongoza timu na Andrew Kazembe chini ya usimamizi wa Michael Malabeja, Injinia James Pilly na Benjamin Mashauri, ambaye ni naibu mkaguzi mkuu.

Kuhusu vifaa vilivyopitwa na wakati na mitambo na miundombinu mikuukuu ya umeme utokanao na maji, ripoti inasema mitambo hiyo ina teknolojia ya zamani kwa kuwa asilimia 70 iliwekwa miaka kumi iliyopita. “Vifaa vya kizamani na mashine zinahitaji kusimikwa upya na matengenezo ya mara kwa mara, la sivyo uendeshaji unakuwa na gharama kubwa kuliko kuendesha mashine au mitambo mipya,” inasema ripoti hiyo ya CAG.

“Kama hakutakuwa na matengenezo sahihi, kuna hatari ya kupoteza zaidi ya asilimia 52 ya uwezo wa jumla wa kuzalisha umeme katika gridi ya Taifa kwa kuwa matengenezo yasiyo sahihi na fanisi yanaweza kuathiri mitambo mingi zaidi.”

Kuhusu zabuni kutotekelezwa, ripoti ya CAG inaonyesha katika mwaka wa fedha wa 2017/18 ambazo hazikutekelezwa kutokana na kutokuwepo kwa fedha za kutosha zilikuwa za thamani ya Sh2.308 trilioni kwa mujibu wa idara na badala yake zilihamishiwa katika mpango wa manunuzi wa mwaka uliofuatia.

Pia ripoti hiyo imeonyesha makisio tofauti ya bajeti ya manunuzi, katika baadhi ya vituo kuwa makubwa yanayofikia asilimia 99 kwa mtambo wa Kidatu na makisio ya chini kwa asilimia 116 kwa mtambo wa Mtera.