CAG abaini upungufu wa Sh7 bilioni usimamizi wa ankara za matibabu nje ya nchi

Tuesday April 16 2019

 

By Herieth Makwetta, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imebaini upungufu katika usimamizi wa ankra za matibabu nje ya nchi kiasi cha Sh7 bilioni.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni Aprili 10,2019 imebaini ukaguzi uliofanywa katika Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zaidi ya Sh7 bilioni zilitumika kwenye matibabu katika Hospitali ya AHEL-India bila kuwa na uthibitisho kwa kiwango kinachoridhisha.

Imebaini ankra zilizowasilishwa zinapingana na aya ya 2 ya kifungu cha 2.2 cha makubaliano kati ya AHEL na MOHS (Kwa sasa MHCDGEC) kinachotaka mgonjwa kuruhusiwa AHEL baada ya kupokea nakala ya barua ya kibali inayotolewa na MHCDGEC.

Katika ripoti hiyo ya CAG, Profesa Mussa Assad amesema kwa kawaida mgonjwa atakayetibiwa anapaswa kuwa na nakala ya barua ya kibali ili AHEL waweze kutumia kibali hicho kuhakiki sifa za wagonjwa.

“Kwa lengo la udhibiti, baada ya kumaliza matibabu wagonjwa wanapaswa kusaini ankra zao kabla ya kurejea Tanzania mara tu baada ya kuruhusiwa. Kwa kuongezea, kwenye ankra ambazo hazikusainiwa, madai mengine hayakuhakikiwa na kamati ya ufundi ya ukaguzi wa kitabibu,” ameeleza CAG.

Upungufu ulioibuliwa ni pamoja na ankra ambazo hazikupitiwa na timu ya wakaguzi wa kitabibu ni Sh3 bilioni.

Ankra ambazo hazikusainiwa na wagonjwa Sh3 bilioni, ankra zisizo na viambatisho Sh121 milion na ankra ambazo hazikuingizwa kwenye rejista Sh59 milioni na kufanya jumla yake kuwa Sh7 bilioni.

Ripoti hiyo imeonyesha hapakuwa na nyaraka toshelezi na kutoingiza ankra kwenye rejista ya wizara.

 

Baada ya ukaguzi huo, barua ya upungufu wa MHCDGEC ya mwaka 2017/2018 wizara ilijibu kuwa imewaagiza matabibu ambata kusimamia udhibiti kwa kuhakikisha kuwa ankra zote zinasainiwa kulingana na tarehe za kuruhusiwa wagonjwa na kwamba zile ambazo hazina viambatisho menejimenti iliahidi kuziwasilisha kwa ajili ya uhakiki.

“Menejimenti haikufanyia kazi mapendekezo yangu ya miaka ya nyuma, kwani ankra za matibabu zinaendelea kujirudia bila kuwa na mkakati wa kuziepuka.”

“Kwa maoni yangu, naamini kuwa kushindwa kuwajibika kwenye matibabu nje ya nchi kunaweza kutengeneza mianya ya matumizi mabaya ye fedha za umma kupitia madai hewa kwa gharama ya mlipa kodi, hivyo thamani ya fedha haiwezi kufikiwa,” anaeleza CAG na kuongeza:

“Hivyo, nashauri menejimenti ya MOHCDGEC kuhakikisha kuwa ankra zote zinapitiwa kitaalamu na kiueledi na maofisa tabibu. Aidha, timu ya ukaguzi wa kitabibu kabla ya malipo ihakikishe kwamba madai yote yasiyo ya kweli yanaondolewa.”

 “Pia ufuatiliaji wa ankra/hati za madai ambazo zinakosekana kutafutwa na ankra zote za kweli na kumbukumbu zake zinaingizwa kwenje rejista ya ankra. Madai yote yaliyohojiwa yanapaswa kuwasilishwa ipasavyo kwa ajili ya uhakiki.”

Advertisement