UCHOKOZI WA EDO : CAG kafika Dodoma kabla ya Mzee Membe kufika Lumumba

Muktasari:

  • Niliwaza jinsi ambavyo Membe angetinga pale akiwa na suti maridadi. Labda na mpambe mmoja au wawili nyuma yake. Niliwaza jinsi ambavyo watakuwa wakitabasamu na katibu wake na ambavyo angemwelekeza ofisi yake ilipo (wanasema maisha bila ya unafiki hayaendi).

Niliwahi kuwaza jinsi mwanasiasa anayeitwa Bernard Membe atakavyokwenda pale Mtaa wa Lumumba katikati ya jiji la Dar es Salaam. Mwishoni mwa Novemba mwaka jana wakati tukikaribia kuuga mwaka aliitwa pale na katibu mkuu wa chama chake.

Niliwaza jinsi ambavyo Membe angetinga pale akiwa na suti maridadi. Labda na mpambe mmoja au wawili nyuma yake. Niliwaza jinsi ambavyo watakuwa wakitabasamu na katibu wake na ambavyo angemwelekeza ofisi yake ilipo (wanasema maisha bila ya unafiki hayaendi).

Jinsi ambavyo waandishi wa habari wangeambiwa wawapishe wakubwa wazungumze. Sitaki kutabiri jinsi ambavyo maongezi yao yangekwenda. Sijui Mzee Membe jasho lingemtoka au ni katibu wake ndiye angetokwa na jasho. Ngumu kujua kwa sababu hata mashtaka yenyewe hatuyaelewi vyema.

Tungesubiri kuona wawili hao wakitoka ofisini na kukutana na waandishi wa habari. Lazima wangekuwa wanatabasamu tu (maisha bila ya unafiki hayaendi). Mwishowe kabisa wangetoa kauli nzuri za kidoplomasia jinsi maongezi yalivyokwenda vyema. Tusingejua nani ametokwa na kijasho chembamba ofisini. Bahati mbaya yote haya yameishia ndotoni. Mpaka leo Mzee Membe hajaenda Lumumba. Nasikia kuna chenga nyingi ndani yake, waliomuhitaji kama vile hawamtaki tena. Nilisikia mwenezi akisema kesi imefungwa. Kitu cha ajabu kidogo. Kesi ilifunguliwa na katibu hadharani huku kukiwa na mashtaka ndani yake, lakini haikusikilizwa, tuendelee kusubiri huenda ikarudi tena.

Ninachojua ni kwamba wakati tukisubiri umbea wa Membe, CAG aliitwa Dodoma akajieleze kwa kauli zake ‘zisizofaa’ dhidi ya Bunge akiwa nje ya nchi. Aliitwa wiki mbili zilizopita, juzi alikuwa na suti yake maridadi pale Dodoma. Nilitamani kilichotokea kwa CAG kingetokea kwa Membe lakini haikuwa.

Kama kesi ya Membe ikiishia njiani tutasikitika sana. Sisi tulioishia darasa la saba tulihitaji kuona kesi zenye mwisho. Huwa tunajifunza kitu kuhusu mambo yanayoizunguka nchi yetu. Wakati mwingine katika madai mazito kama yale huwa tunahitaji kuona watu wanaomhujumu Namba Moja wanavyoadabishwa mchana kweupe.

Vinginevyo kama hakukuwa na kesi basi udadisi wetu unazidi kuelea. Labda ni wakati wa kutafakari mambo kabla ya kuyasema. Inawezekana kuna watu wanatoa kauli halafu ndio wanatafakari. Labda katibu aliongea kwanza halafu akatafakari kisha akafuta mashtaka kimya kimya.