CBA, M-Pawa watangaza bingo ya Sh15 milioni

Thursday June 13 2019

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya Vodacom kutangaza kuwapeleka wateja 10 kushuhudia michuano ya Afcon yatakayofanyika nchini Misri, huduma yake ya M-Pawa kushirikiana na Benki ya CBA inaendesha bahati nasibu itakayotoa zawadi ya Sh15 milioni.

Licha ya zawadi hiyo itakayotolewa kwa mshindi wa jumla, wateja wengine 2,000 wa huduma hiyo inayotimiza miaka mitano tangu ianzishwe watapata zawadi mbalimbali.

Akizindua promosheni hiyo, mkurugenzi mtendaji wa Benki ya CBA, Gift Shoko amesema itafanyika kwa wiki sita na droo ya kwanza itatoa washindi 340 ambao 40 kati yao watazidishiwa mara mbili ya akiba waliyonayo kwenye akaunti zao kuanzia  Sh1,000 hadi Sh200,000 na wengine 300 watashinda muda wa maongezi wa Sh5,000 kila mmoja.

“Promosheni itaendelea na kila wiki kutakuwa na washindi 50. Mshindi mkubwa atatangazwa kwenye droo ya mwisho na atajinyakulia Sh15 milioni,” amesema Shoko.

Huduma ya M-Pawa inayotolewa na benki hiyo kwa kushirikiana na Vodacom ilizinduliwa miaka mitano iliyopita kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya huduma za fedha hasa kwa wafanyabiashara wadogo na wananchi wa vijijini ambao hawajafikiwa.

Kwa sasa, zaidi ya asilimia 65 ya Watanzania wanapata huduma za fedha wengi wakitumia simu zao za mkononi zinazowaruhusu kutunza, kuhamisha au kutoa mahali popote walipo.

Kwa wateja wanaopenda kushiriki promosheni hiyo, Shoko amesema washindi watachaguliwa kwa kuzingatia utunzaji fedha kwenye akaunti ya M-Pawa au ulipaji deni kwa waliokopa na yeyote mwenye sifa hizo na akiba ya kuanzia Sh1,000 mpaka Sh200,000 ataongezewa mara mbili katika droo za kila wiki zinazosimamiwa na wawakilishi kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) pamoja na zawadi nyinginezo.

 


Advertisement