CCM, Ukawa kupokezana unaibu meya Dar

Friday December 7 2018

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya mvutano na majibizano ya hapa na pale hatimaye Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam limekubaliana kuachiana nafasi ya unaibu meya kwa awamu.

Hatua  hiyo inafanya kuwa naibu meya wa CCM atakaa katika nafasi hiyo kwa miezi mitatu kisha yule wa CUF anayetokana na Ukawa naye atakaa kwa kipindi hicho.

Hata hivyo, haikuwa kazi rahisi kwa makubaliano kufikiwa kutokana kila upande kuwa na msimamo wake wenye masilahi kwa chama chake huku idadi wajumbe ikiwa sawa 12 kwa 12.

Chanzo cha mabishano hayo inadaiwa ni hatua ya Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana kutangaza kuwa uchaguzi ufanyike lakini mgombea atakuwa ni mmoja wa CCM katika nafasi ya unaibu meya.

 Kauli iliwaamsha  baadhi ya wajumbe wa Ukawa, wakiongozwa na SaedKubenea, Boniface Jacob kusimama na kuomba utaratibu kisha kusema  jambo haliwezekani kwa kile walichodai kuwa Sipora amekiuka makubaliano.

“ Mkurugenzi jambo hili haliwezekani, kwa sababu katika kikao cha mwisho tulikubaliana kuwa uandikie barua kwa vyama kwa ajili ya kuteua wagombea.Leo (jana) unatuambia mgombea ni mmoja tuelewe lipi.

“Barua haujaandika na siku ulidai mgombea wa CUF alichelewa kuwasilisha jina lake katika ofisi yako kwa mujibu wa taratibu. Ndio maana Dk Ndugulile (Faustine- mjumbe) alitumia busara ya kushauri vyama viandikiwe barua, lakini suala la uchaguzi unalotaka halifanyiki hapa,”

Kauli hiyo ya Jacob ambaye ni meya wa Ubungo iliwaamsha baadhi ya  wajumbe wa CCM waliotaka uchaguzi huo uendelee kama kawaida na mgombea wa Mariam Lulida apigiwe kura kwa kuwa yupo peke yake.

Hata hivyo, malumbano yaliendelea ndipo mjumbe mwingine wa CCM  Abdallah Chaurembo aliposimama na kusema; “ Mheshimiwa mwenyekiti na kusema huu uchaguzi ni vyema ukaahirishwa kwa sababu maandalizi yake hayapo sawa. Tukisema tuendelee na hali hii iliyopo hatutapata muafaka.”

Maelezo hayo ya Chaurembo yaliungwa mkono na wajumbe wa Ukawa, lakini muda mfupi Sipora aliwasha kipaza sauti na kusema; “ Uchaguzi lazima ufanyike kwa sababu hakuna fedha za posho kwa vikao vingine.”

Kauli hiyo iliibua upya minong’ono miongoni mwa wajumbe wa Chadema nakusababisha zogo kwa kila mtu kuongea bila kupewa ruhusa. Mwenyekiti wa kikao hicho, alikuwa Isaya Mwita.

Lakini, baada ya muda Sipora alishika kipaza sauti na kusema baada ya kushauriana na mwanasheria wa jiji hilo, wameamua kutumia jina la mgombea wa CUF lililowasilishwa wakati huo,

 Hata hivyo, wajumbe wa Ukawa hawakukubaliana naye na  Kubenea alipopewa nafasi alitoa ushauri wa kugawa awamu za uongozi katika nafasi hiyo kulingana na hali halisi na sintofahamu iliyojitokeza.

Pia, mjumbe wa CCM Benjamin Sitta naye alitoa ushauri akitaka wakae kama kamati kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa sintofahamu hiyo.

 Mwita alikubaliana na jambo hilo na wajumbe hao baada ya kurudi kwa dakika kadhaa alitangaza kuwa wamekubaliana kuachiana na nafasi hiyo na mchakato huo utaanza Desemba 30 hadi Juni 30 mwakani.

“ Tumeamua kukubaliana na jambo hili kwa masilahi ya wananchi wa Dar es Salaam na kuhusu nani ataanza hilo niachie mimi kwa sababu nitakutana na manaibu meya wangu na kupanga,” alisema Mwita.

Wakizungumza baada ya mchakato huo kukamilika manaibu meya hao waliwashukuru wajumbe wa baraza hilo kwa kufikia uamuzi ambao utakuwa na manufaa katika jiji la Dar es Salaam.

“ Nashukuru utaratibu na kanuni zilizotumika hadi kufikia hatua hiii. Kikubwa ni ushirikiano naomba kutoka kwenu,”alisema Haroub Othman diwani wa Kata ya Makumbusho (CUF)

Naye Lulida (CCM-Kata ya Mchafukoge) alisema; “Nawashukuru wote ninawahidi kuwa mchapakazi.”


Advertisement