Ukawa: CCM wajiandae kwa anguko 2015

Saturday November 15 2014Viongozi wa Ukawa Tanzania

Viongozi wa Ukawa Tanzania 

By Mwinyi Sadallah Mwananchi

Zanzibar. Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Zanzibar wameibeza ripoti iliyotolewa wiki hii na Taasisi ya Twaweza, wakisema haielezi hali halisi ilivyo.

Wamesema kwamba kutokana na ukweli huo, CCM iwe tayari kupokea matokeo magumu ya anguko katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani.

Tamko hilo limetolewa na viongozi wa vyama vinavyounda umoja huo, walipozungumza gazeti hili kwa nyakati tofauti, kufuatia ripoti ya utafiti ya Twaweza, inayoonyesha kuwa Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa anaongoza kati ya wagombea wanaotajwa kama uchaguzi ungefanyika sasa.

Makamu mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi Haji Ambari Khamis alisema kwamba muungano huo unakwenda na ajenda tatu katika kampeni za Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa na uchaguzi mkuu wa mwakani.

Alizitaja ajenda hizo kuwa ni pamoja na tatizo la umaskini, kudhrauriwa kwa Katiba ya wananchi, kuongezeka rushwa na ufisadi hali inayoathiri wananchi wa pande zote mbili za muungano.

“Kama mipango na mikakati itakwenda bila ya kujitokeza mabadiliko, CCM watakuwa na wakati mgumu kwa nafasi zote za wagombea ikiwemo urais wa Muungano na Zanzibar,” alisema Ambari ambaye pia aligombea urais wa Zanzibar mwaka 2010.

Advertisement

Upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Zanzibar (Chadema), Said Issa Mohamed alisema kuwa Ripoti ya Twaweza inapotosha ukweli dhidi ya nguvu za Ukawa katika kuelekea uchaguzi wa mwakani.

Alisema kwamba kutokana na kazi kubwa iliyofanywa na Ukawa tangu kuasisiwa ni wakati mwafaka kwa viongozi na wanachama wa CCM kuanza kujitayarisha kisaikolojia ili kukubali matokeo magumu yatakayowakumba mwakani.

Hata hivyo, alisema katika ripoti hiyo kuna mambo ya msingi wanayokubaliana nayo ikiwamo kuongezeka kwa umaskini uliofikia asilimia 63 kutoka 49.

Pia, alitaja kuongezeka kwa matatizo ya huduma za afya pamoja na kuporomoka sekta ya elimu hadi kufikia asilimia 38 kutoka 46 mwaka 2012.

Alisema iwapo kuna asilimia 33 ya wananchi hawajaamua wampigie kura mgombea yeyote kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ukawa inaamini watu hao watakuwa wamepata msimamo huo kutokana na kazi inayoendelea kufanywa na Ukawa ya kutoa elimu ya uraia kuhusu kasoro za Katiba Inayopendekezwa na sababu za kuongezeka umaskini nchini.

Mkurugenzi wa Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salim Bimani Abdalla alisema kuwa utafiti wa Twaweza una kasoro nyingi, licha ya kueleza matatizo ya umaskini na kuanguka kwa sekta muhimu za huduma za jamii.

Alisema kuwa Twaweza imeshindwa kueleza sababu za kuongezeka kwa umaskini wakati taifa linakabiliwa na tatizo la rushwa na ufisadi.

Alisema kwamba ni kweli Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa ana mvuto na kukubalika kwa wananchi wa pande mbili za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kati ya wagombea wanaotajwa wa CCM, lakini bado kikwazo kikubwa kipo ndani ya chama chake.

Alieleza kuwa iwapo Lowassa hatapitishwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais, anguko litamkuta mgombea yoyote wa CCM kutoka kwa mgombea wa muungano wa Ukawa.

“Ripoti ya Twaweza sawa na hawawezi kwa sababu wanashindwa kusema ukweli kuhusu nguvu za Ukawa wakihofia masilahi yao,” alisema Bimani.

Hata hivyo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema kuwa ni mapema kuzungumzia Ripoti ya Twaweza kwa sababu chama chake hakijakaa na kuichambua.

“Kama chama, bado hatujakaa kutathimini Ripoti ya Twaweza, lakini kabla ya matokeo ya ripoti, CCM tunajua tunashinda Tanzania Bara na Zanzibar katika uchaguzi wa mwakani,” alisema Vuai.

Alisema kwamba sababu kubwa ya kushinda katika uchaguzi huo ni Serikali ya CCM kufanya vizuri katika utekelezaji wa Ilani yake ya uchaguzi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka 2010.

Advertisement