CCM yataja mtaji wa kura za 2020

Muktasari:

CCM imeanza hesabu ya kuingia na mtaji wa nusu ya kura katika Uchaguzi Mkuu wa 2020 ambazo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema zitapatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayogusa maisha ya wananchi moja kwa moja

Bukoba. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema CCM lazima ijiridhishe ina nusu ya kura au zaidi kuelekea uchaguzi mkuu na itapatikana kwa kunadi mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano.

Amekariri kauli yake kuhusu ugumu waliopata wa kunadi ilani ya CCM mwaka 2015, kuwa hawako tayari kuingia mwaka 2020 na viongozi wabovu na baadaye wahangaishwe na mtu wanayemjua.

Akifungua kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Kagera leo Februari 21, 2019 mjini Bukoba, Waziri Mkuu amesema nusu hiyo ya kura itapatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.

Amesema Serikali imejikita kwenye maeneo muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja na kuwa ni wajibu wa viongozi kufuatilia utekelezaji umefanyika kwa kiwango gani katika maeneo yao.

"Leo tuna miaka mitatu, chama lazima kijiridhishe angalau tuna nusu ya kura tunazozihitaji au zaidi, tumejikita kwenye maeneo muhimu ambayo yanagusa wananchi moja kwa moja," amesema Majaliwa.

Pia amewataka wakurugenzi wa halmashauri kutoa taarifa kwenye vikao vya chama kwamba wajumbe wanataka kujua utekelezaji wa mambo yanayotekelezwa katika maeneo yao.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amepewa jukumu la kulea mikoa ya Kigoma na Kagera kichama ametaka uwe mwisho wa misuguano iliyokuwa inaendelea kwenye chama hicho.

Amewataka kujipanga kwa uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na kufanya tathmini ya maeneo waliyopoteza na kuandaa wagombea watakaoweza kukomboa maeneo waliyopoteza katika uchaguzi uliotangulia.

Kuhusu zao la kahawa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema msimu wa mwaka jana ulikuwa na lawama na kutaka changamoto zilizojitokeza zifanyiwe kazi kabla ya msimu mpya kuanza na mfumo uangaliwe kuanzia kwa mkulima hadi kwenye soko.