CCM yatoa vigezo vya kuwapata wagombea 2020

Sunday November 25 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Morogoro. Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro kimesema kupatikana kwa wagombea wa udiwani na ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kutatokana na ushiriki wao katika shughuli za maendeleo ya chama hicho.

Pia, kimesema hadhi wanayopata wabunge ambao baadhi yao huteuliwa kuwa mawaziri au naibu waziri na madiwani wakiwa wenyeviti wa halmashauri au mameya inatokana na heshima ya CCM kukubalika kwa wananchi.

Hayo yalielezwa jana Jumamosi Novemba 24, 2018 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Morogoro, Innocent Karogelesi alipokuwa akifunga mafunzo ya siasa, itikadi na maadili kwa vijana wa chama hicho Kilosa mkoani humo.

Karogelesi alisema chama ndicho kinachowapa tiketi wanachama wake kugombea ubunge na udiwani hivyo wanapochaguliwa hawapaswi kujiweka mbali na shughuli za ujenzi wa CCM.

Alisema hakuna mwanafunzi anayeweza kujivunia kufanikiwa kwake kielimu ikiwa hawezi kutambua au kuheshimu mchango mkubwa uliotolewa na walimu wake ama katika masomo ya awali au shule ya msingi.

"Ili tuwapitishe wagombea wetu kwenye udiwani au ubunge mwaka 2020, tutampima kila mgombea kutokana na ushiriki wake katika kazi za chama bila kumtazama usoni.”

Advertisement

“Sifa ya msingi na ya awali nje ya uanachama wake ni kujihusisha kwake na maendeleo ya CCM," alisema Karogelesi.

Mwenyekiti huyo alisema chama cha siasa kitakachokosa kujijenga, kuimarika na kukubalika hakitapata madiwani na wabunge hivyo hata rais atashindwa kuteua mawaziri na naibu wake.

Alisema kwenye majiji na halmashauri hakutakuwa na wenyeviti au mameya wa CCM.

Aliwataka wabunge wa kuchaguliwa, madiwani na wale wa viti maalumu kutambua kufika kwao walipo sasa kumetokana na nguvu ya chama na si uwezo wao binafsi.

Karogelesi aliwataka wanachama wa CCM na jumuiya zake kutambua wana wajibu na ulazima wa kuishi kwa kuheshimu misingi ya chama kikatiba, kinidhamu na kimaadili ili kila kiongozi haiba yake iwe ni kioo kinachoakisi mema kwa chama na jamii.

Mwenyekiti huyo alimuagiza Katibu wa CCM mkoa huo, Shaka Hamdu Shaka, kuwaandikia barua ya ukumbusho wabunge na madiwani wote juu ya ushiriki na wajibu wao ndani ya chama na kwenye jamii.

Pia, makatibu wote wa CCM na jumuiya zake mkoani aliwataka kutoa maelekezo na kuwataka wanachama wao kujiweka mbali na vitendo vya udalali wa kisiasa na rushwa.

Advertisement