CCM yawataka mabalozi wake kutanganza mazuri ya chama

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally

Muktasari:

  • CCM yashuka kwa mabalozi kuweka mikakati kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, wapewa semina ya kujiimarisha

Dar es Salaam. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kinondoni kimeanza mikakati ya ndani ya kujiimarisha na kuhakikisha kinafanya vizuri kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotatajiwa kufanyika mwaka huu.

Leo Jumapili Juni 23, 2019, chama hicho kimefanya semina kwa mabalozi wa CCM wilayani humo iliyolenga kuwajengea uwezo na kuweka mikakati ya kuhakikisha kinaendelea kushika dola.

Akifungua semina hiyo, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amewataka mabalozi kuwa vinara wa kutangaza mambo mazuri yanayofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

Amesema mabalozi ndiyo walio karibu zaidi na wananchi hivyo wanatakiwa kuwaonyesha mafanikio yaliyopatikana na kazi kubwa inayoendelea kufanywa.

“Ushindi wa CCM unaanzia kwa mabalozi, ukitaka kujua uongozi ndani ya CCM anza kuwatazama mabalozi. Niwasisitize tu kuna mambo yamefanyika kuanzia kwenye afya, elimu hadi kutetea haki za wanyonge mkayazungumzie haya kwa watu,”

Dk Bashiru amesema anafahamu kuna watu wanapotosha kazi nzuri inayofanywa na serikali hivyo ni jukumu la mabalozi na vijana wa CCM kuzungumza ukweli.

“Wapo wanaotumia mitandao ya kijamii kupotosha, vijana wa CCM ingieni huko mueleze ukweli, toeni ufafanuzi watu waelewe ukweli na sio maneno ya upotoshaji,” amesema.

Katibu Mkuu huyo pia amegusia suala la vijana wa chama hicho na kueleza kuwa hawafanyi shughuli za kijeshi kama inavyoelezwa bali wanatumika kwa ajili ya hamasa na protoko.

“Hatuna haja ya kikundi cha kijeshi tunayo JWTZ, polisi hao wote wana kazi ya kuhakikisha ulinzi na usalama. Vikundi vya vijana tulio nao CCM ni wa hamasa na protoko hawa wana kazi ya kuweka kwenye utaratibu,”