CRDB, UBA zaidhamini Serikali mradi wa umeme Rufiji

Monday April 15 2019

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Ili kufanikisha kuanza kwa ujenzi wa mradi wa umeme katika Bonde la Mto Rufiji, Benki ya CRDB kwa kushirikiana na UBA zimekabidhi mkataba wa kuidhamini Serikali.

Makubaliano hayo yameridhiwa leo, Aprili 15, 2019 kwa benki hizo kuahidi kutoa Sh1.7 trilioni (Dola 737.5 milioni) mbele ya wawakilishi wa Serikali, mkandarasi pamoja na watendaji Tanesco jijini Dar es Salaam jambo linalomaanisha kukamilika kwa mchakato wa kuandaa rasilimali fedha zinaohitajika.

Akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano hayo, mkurugenzi mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema ni furaha kwao kufanikisha mradi huo wa ipaumbele utakaokuwa na manufaa kwa Taifa.

“Hii si mara ya kwanza kwa CRDB kushiriki wenye miradi mikubwa ya Serikali. Tulitoa mchango wetu kwenye ujenzi ya reli ya kisasa (SGR) na usambazajiwa umeme vijijini (Rea) na sasa tumepata heshima kubwa kufanikisha ujenzi wa Stiepgler’s Gorge,” amesema Nsekela.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa Benki ya UBA, Usman Imam Isiaka amesema kwa mara ya kwanza Tanzania imeweka historia kwa benki zake za ndani kudhamini mradi wa fedha nyingi kiasi hicho.

Isiaka alifafanua kuwa kufanikisha utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa umeme utakaogharimu Sh6.6 trilioni (Dola 2.95 bilioni), walihitajika wadhamini wa ndani kwa asilimia 30 na kimataifa kwa asilimia 70.

“Katika Dola 737.5 milioni kuna Dola 516 milioni ambazo ni udhamini wa fedha za kigeni ambazo kila benki itatoa asilimia 50 na Dola 221 milioni zinazobaki ni kwa Shilingi ya Tanzania ambazo CRDB watatoa asilimia 51 na sisi asilimia 49,” amesema Isiaka.

Benki za nje zitakazofanikisha mradi huo amesema ni Benki Kuu ya Misri pamoja Benki ya Afriexim zitakazotoa dhamana ya asilimia 70 ya fedha zote za kufanikisha mradi huo.

Naibu gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Bernard Kibesse amesema wamejipanga kuzisimamia benki hizo kuhakikisha zinafanikisha miamala hiyo muhimu kwa mradi huo utakaozalisha umeme wa kukidhi mahitaji yote nchini pindi utakapokamilika.

  “Tumejenga reli ya kisasa na tuna hazina kubwa ya madini ya chuma huko Liganga na Mchuchuma ambayo inahitaji umeme nafuu kufanikisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali kama vile magari na vipuri vyake,” amesema Dk Kibesse.

Utakapokamilika, mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 2,100 ambazo ni zaidi ya megawati 1,500 zinazohitajika nchini kwa mwaka mzima.

Advertisement