CT Scan zaanza kufungwa Temeke, Mwananyamala na Amana

Muktasari:

Uamuzi  wa kufunga mashine hizo unatokana na huduma za SC Scan na MRI kutokuwepo katika hospitali za rufaa za Mikoa.


Dodoma. Serikali ya Tanzania imeanza kutekeleza ufungaji wa mashine za CT Scan katika Hospitali za rufaa za Mikoa za Mwananyamala, Temeke na Amana.

Imesema uamuzi huo unatokana na mwongozo uliotokana na   huduma za CT Scan na MRI kutokuwepo kwenye hospitali za rufaa za Mikoa.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Juni 11, 2019 bungeni jijini Dodoma na naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la mbunge wa Viti maalum (CCM), Mariam Kisangi aliyetaka kujua mpango wa Serikali kupeleka vipimo vya MRI katika hospitali hospitali hizo tatu za jijini Dar es Salaam.

“Wizara ya Afya  ilifanya mabadiliko ya mwongozo wa kutengeneza mwongozo wa vifaa vya radiolojia nchini wa mwaka 2018, pamoja na mambo mengine huduma za CT-Scan sasa zitapatikana katika ngazi ya Hospitali za rufaa za mikoa na huduma za MRI zitapatikana katika ngazi ya hospitali za rufaa za kanda na Taifa,” alisema Dk Ndugulile.