CUF Pemba wataka bendera za ACT

Muktasari:

Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kusini Pemba nao waanza kuunga mkono uamuzi wa Maalim Seif Sharif Hamad kuhamia ACT- Wazalendo baada ya leo Jumanne kuanza kushusha bendera za CUF na kupandisha mpya za ACT- Wazalendo.

Pemba. Harakati za ubadilishwaji wa bendera katika matawi mbalimbali ya Chama cha Wananchi (CUF) kisiwani Pemba zinaendelea asubuhi hii na kupandishwa za ACT- Wazalendo huku wakitaka bendera hizo haraka kisiwani humo.

Katika wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba matawi mbalimbali yanaendelea kubadilishwa bendera hizo na wananchi walio wengi wanaonekana ni wenye kufurahia  hatua hiyo.

Shughuli hiyo ya ubadilishwaji wa bendera inaongozwa na Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Micheweni, Rashid Khalid Salim akiwa pamoja na waliokua viongozi wa chama chao awali.

Kwa mujibu wa Salim wanachokifanya sasa ni kubadili bendera maeneo yote na kufungua matawi mengine mapya ya ACT- Wazalendo kwenye wilaya yao.

Amesema kwa sababu jambo hili limetokea kwa kipindi kifupi na baadhi ya walio wengi hawakuwa wamejipanga kufanya hivyo ndio maana maeneo mengine kuna ukosefu wa vifaa zikiwemo bendera na rangi.

Kutokana na hali hiyo Salim aliwataka viongozi wakuu wa chama hicho kuhakikisha wanawapatia bendera za ACT-Wazalendo haraka.

Kwa upande wake aliyekua mwakilishi wa CUF Jimbo la Micheweni, Thubeit Khamis Faki amesema hawana muda wa kupoteza na kujadiliana kuhusu kumuunga mkono Profesa Ibrahim Lipumba kwa sasa wanachokiangalia ni kusonga mbele.

Alipoulizwa kuhusu majengo ya ofisi za CUF wanaamuaje kufanya mabadiliko amesema majengo mengi ya ofisi za chama ni ya wananchi wenyewe waliojitolea hivyo si miongoni mwa mali za chama hicho.