CUF Zanzibar wakataa uongozi mpya

Mwandishi Wetu. Baadhi ya viongozi na wafuasi wa CUF visiwani Zanzibar ambao wanamuunga mkono Maalim Seif Hamad wamepinga kitendo cha Profesa Ibrahim Lipumba na wafuasi wake kuitisha mkutano mkuu na kufanya mabadiliko ya katiba na viongozi.

Mkutano huo ulimchagua tena Lipumba kuwa mwenyekiti na kumpa mamlaka ya kuteua katibu mkuu na manaibu wake.

Lakini wafuasi wa CUF, ambayo ina nguvu visiwani Zanzibar wamepinga.

“Tunatambua kwamba Lipumba hana watu wanaomuunga mkono hapa Zanzibar, ndiyo maana amechukua watu kutoka maeneo mbalimbali na kuitisha mkutano mkuu kisha kufanya waliyoyafanya,” alisema Fadhili Sijaamini Ali, ambaye ni katibu wa CUF Wilaya ya Mjini.

Sijaamini alisema wanachoshukuru hivi sasa ni kuona jinsi gani Maalim Seif alivyowatuliza wafuasi wa CUF katika kadhia hiyo, akidai kwamba kiongozi huyo ni moja ya viongozi wa mfano mkubwa kisiasa.

“Hivi sasa tunasubiri kauli yake baada ya kujadiliana na viongozi wenzake wa juu kuhusu hatma ya chama chetu kutokana na kuonekana anafanyiwa hujuma kubwa,” alisema.

“Atakachotuambia Maalim Seif tupo tayari kukitekeleza kwa kuwa yeye ndie tunayemuamini na ndio kiongozi halali wa chama chetu hadi wakati huu licha ya kufanyika kwa uchaguzi.”

Nassor Khamis, ambaye ni Katibu wa Jimbo la Kwahani, masikio yake anayaelekeza kusikiliza hatma ya chama hicho.

“Si kusikiliza maneno ya Lipumba,” alisema.

Kiongozi mwingine, Nassom Amini (katibu Jimbo la Malindi), alisema kwa wakati huu hawezi kusema kwa undani juu ya kinachoendelea, ila alisema kwamba ndani ya jimbo lake hakuna tawi hata moja lililotetereka kutokana na uchaguzi uliofanyika mwishoni mwa wiki.

“Kwa kuwa sisi tuna imani na Maalim Seif, huu uchaguzi wa akina Lipumba wala haujatushtua, kwa kuwa matawi yote yanaendelea kufanya kazi zake za kichama kama kawaida,” alisema.

Ame Omar Ame, ambaye ni katibu wa jimbo la Magomeni alisema anayemfuata Lipumba ni mtu mwenye kufuata masilahi ndio maana hawana hofu juu ya upatikanaji wa haki yao chini ya Maalim Seif.

“Hakuna asiyejua kundi zima la Lipumba ni watu wenye kuweka maslahi mbele, wala hawana uchungu na chama. Sisi kwa upande wetu hatuna shaka juu ya kusambaratika chama kutokana na hujuma zinazofanywa.” alisema.

Naye Mohamed Kassim (katibu wa Kikwajuni) alienda mbali zaidi kwa kusema kuwa Lipumba asingefika mbali kama vyombo vya habari vingempuuza.

Alisema kutangazwa mara kwa mara na vyombo vya habari kumempa kiburi cha kufikia hatua hiyo iliyopo hivi sasa, huku akidai kwamba baadhi ya vyombo humtangaza makusudi ili kumkomoa Maalim Seif.

Kwa upande wa katibu mtendaji wa Jumuiya ya vijana (JuviCUF), Mahmoud Mahinda alisema hawataweza kurudi nyuma na wataendelea kusonga mbele hata ikifikia hatua ya Maalim Seif kufukuzwa ndani ya chama.

Alisema wanatambua kinachoendelea ni mchezo mchafu tu, lakini inatambulika wazi kwamba mapenzi na shauku ya wafuasi wa CUF yapo kwa Maalim Seif ambaye alisema ni mtetezi wa wanyonge.

Maneno kama hayo yalisemwa na katibu wa Wilaya ya Chakechake Mkoa wa Kusini Pemba, Saleh Nassor Juma.

Alisema kinachoendelea ni kuvuruga upinzani kwa ajili ya kuirahisishia CCM ushindi mwaka 2020.

Alisema anaamini wanayoyafanya Lipumba na wenzake hayana nia njema wala hawahitaji chama badala yake wanatumika kuua CUF wakijua kuwa ndio chama chenye nguvu visiwani Zanzibar.

Mkurugenzi wa Habari wa CUF upande wa Maalim Seif, Salim Bimani aliiambia Mwananchi kuwa kwa sasa hana jambo la kuelezea kuhusu hatua ya Lipumba kuteua katibu mkuu mpya.

“Naomba tosheka na hapo tu, ya kwamba hatuna la kusema kwa wakati huu,” alisema Bimani.