CUF walinda ofisi zao Zanzibar

Muktasari:

  • Chama cha Wananchi (CUF) imeweka ulinzi kwa ofisi zake za makao makuu ya chama hicho Mtendeni mjini Unguja Zanzibar ili kuhakikisha hakuna mtu anayeingia asiyehusika

Unguja. Katika hali  isiokua  ya kawaida baadhi ya walizi wa Chama  cha Wananchi (CUF) kutoka maeneo tofauti ya Unguja wamezingira makao makuu ya chama hicho yaliopo Mtendeni mjini hapa kwa ajili ya ulinzi.

Uwepo wa hali hio unatokana  na kile kilichokuwa kinasubiriwa kwa hamu na pande mbili zenye mgogoro wa muda mrefu uliokigawa chama hicho.

Pande  hizo ni ile ya Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad na mwenyekiti anayetambulika na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.

Mwananchi ikiwa Mtendeni mjini Unguja imeshuhudia makundi ya walinzi  wa chama hicho wakiwa katika hali ya u tayari huku wengi wao wakionekana ni kutoka maeneo ya shamba tofauti za Unguja.

Alipoulizwa na Mwananchi mmoja wa miongoni mwa viongozi wa chama hicho  Omar Ali Shehe amesema uwepo wa hali hio ni jambo la kawaida ukizingatia usalama wa chama.

Shehe ambae ni Mkurugenzi wa uchaguzi katika chama hicho ameleza chama chao kina mgogoro katika pande mbili hivyo anaamini kwamba lolote linaweza kutokea na ndiyo maana wameamua kuweka ulinzi kupitia vijana wao.

Hata hivyo amewataka wananchi wasishituke na hali hio huku wakisubiri maamuzi ya Mahakama na kile ambacho viongozi wa chama chao watakieleza baada ya vikao halali vya chama .