CUF wasuka kanda kumng'oa rasmi Maalim Seif

Muktasari:

  • Mkutano Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) unaendelea kwa kuwachagua wajumbe wa Baraza Kuu ambalo baadaye baraza hilo litamchagua katibu mkuu wa chama hicho

Dar es Salaam. Wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) wamejifungia tangu jana Jumatano Machi 13, 2019 kuunda kikosi kitakachomng'oa rasmi Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mkutano Mkuu wa chama hicho ulioanza juzi Jumanne Machi 12, 2019 pamoja na mambo mengine ulifanya mabadiliko ya katiba na kuchagua viongozi akiwamo Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti.

Baada ya Profesa Lipumba kuchaguliwa jana, mkutano mkuu huo uliendelea mpaka sasa ambapo wanafanya uchaguzi wa wajumbe wa Baraza Kuu kwa kanda kisha baraza hilo litamchagua katibu mkuu kurithi mikoba ya Maalim Seif

Jana jioni wajumbe hao waliwachagua wajumbe wa baraza kuu wa kanda ya Unguja na Pemba.

Mkurugenzi wa habari wa CUF, Abdul Kambaya akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Machi 14, 2019 amesema kinachoendelea ni kufanya uchaguzi wa wajumbe wa baraza kuu kwa kanda.

Amezitaja kanda hizo ni Kanda ya Nyanda za juu Kusini, Kanda ya Magharibi, Kati, Pwani, Kaskazini na zilizochaguana jana za Unguja na Pemba.

"Baada ya kupatikana wajumbe wa Baraza Kuu, wao ndiyo watamchagua katibu mkuu wa chama," amesema Kambaya

Hatua ya katibu mkuu kupatikana kwa kuchaguliwa na Baraza Kuu inatokana na mabadiliko ya katiba yaliyofanyika juzi ambayo sasa mwenyekiti atateua majina matatu kwa kushauriana na makamu wenyeviti Bara na Zanzibar kisha kuyapeleka katika baraza kuu ambalo litachagua jina moja.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kinachoendelea