Chadema kuipinga sheria ya vyama vya siasa mahakamani

Profesa Abdallah Safari 

Muktasari:

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitafungua kesi mahakamani kupinga muswada wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo sasa unasubiri kusainiwa na Rais  John Magufuli ili kuanza kutumika

 


Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kitafungua kesi mahakamani kupinga sheria ya vyama vya siasa ambayo sasa unasubiri kusainiwa na Rais  John Magufuli ili kuanza kutumika.

Akizungumza leo Ijumaa Februari 15, 2019 makamu mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdallah Safari amesema chama hicho kilipinga muswada huo lakini kesi yake ya kuupinga haikusajiliwa mahakamani.

"Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa (wa mwaka 2018) unakuja kunyonga demokrasia, tulishirikiana na wadau kuupinga lakini hatukufanikiwa sasa tutafungua kesi ya kupinga sheria yenyewe itakapoanza kutumika,” amesema Profesa Safari.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji amesema chama hicho kinasubiri sheria hiyo itangazwe katika gazeti la Serikali (GN) ili kupeleka mahakamani vipengele ambavyo hawajaridhishwa navyo.

"Mahakama ina mamlaka ya kuondoa vipengele vyote ambavyo vinaminya haki za binadamu lakini pia vinavyokiuka katiba ya nchi. Hata tulipokwenda kusajili kesi ya kupinga muswada tuliambiwa tusubiri iwe sheria," amesema Dr Mashinji.

Profesa Safari pia aligusia muundo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), akisema kuwa unatakiwa kuboreshwa  akibainisha kuwa chama hicho kikuu cha upinzani nchini kinatarajia kuandaa rasmi muundo wa tume hiyo kwa kushirikiana na wadau wengine, vikiwemo vyama vya siasa kwa lengo la kuibua mjadala wa kitaifa.