Chadema waiangukia mahakama rufaa ya Mbowe, Matiko

What you need to know:

Chadema kimezungumzia rufaa ya mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na mhazini wa Baraza la Wanawake (Bawacha), Esther Matiko na kuiomba mahakama kumaliza mapema kesi inayowakabili ili warudi kuwatumikia wananchi na Taifa


Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimezungumzia sakata la kufutiwa dhamana kwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko kikiiomba Mahakama kumaliza mapema sakata hilo ili washtakiwa hao waendelee na shughuli zao za kibunge.

Kimesema Mbowe na Matiko kuendelea kuwa mahabusu kinawafanya wananchi waliowachagua na Taifa kukosa uwakilishi wao katika maeneo mbalimbali.

Novemba 30, 2018  Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ilisimamisha usikilizaji Rufaa ya Mbowe na Matiko hadi rufaa ya Serikali itakapoamuliwa na Mahakama ya Rufani.

Mbowe na Matiko watasubiri Mahakama ya Rufaa kupanga siku ya kusikiliza rufaa hiyo na hivyo kurejeshwa mahabusu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Desemba 5, 2018 naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John Mnyika amesema wananchi wanakosa uwakilishi wa Mbowe na Matiko.

“Nchi imekosa uwakilishi wa kiongozi wa michezo ya wabunge wanawake inayoendelea nchini Burundi kwa kuwa kiongozi huyo (Matiko) yuko ndani kwa kukosa dhamana baada ya kwenda (Burundi) kuwawakilisha wenzake,” amesema Mnyika.

Mnyika ameiomba mahakama ya Rufaa kupitia majalada yote ya kesi, kuanzia Mahakama ya Kisutu pamoja na rufaa zote za Mahakama Kuu ili kuangalia uwezekano wa kumaliza kesi hiyo mapema.

“Tunafahamu majaji wanakaribia kwenda likizo tumeiandikia Mahakama ya Rufaa iziite pande zote mbili na kupitia mwenendo mzima wa kesi,  kuanzia ilipofunguliwa hadi rufaa zote za Mahakama Kuu ili kuangalia uwezekano wa kumaliza kesi hii,” amesema Mnyika.

Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana hiyo Novemba 23, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri baada ya maombi ya upande wa mashtaka, kwa madai ya kukiuka mashaty ya dhamana kwa kutofika  mahakamani tarehe ambazo kesi yao ilipangwa kwa usikilizwaji wa awali.

Baada ya kufutiwa dhamana hiyo walikata rufaa Mahakama Kuu, kupinga uamuzi huo.

Kabla ya rufaa hiyo. Serikali iliweka pingamizi la awali ikiomba mahakama iitupilie mbali rufaa hiyo kwa madai kuwa ina kasoro za kisehria.

Mahakama Kuu licha ya kukubaliana na baadhi ya hoja za pingamizi la Serikali, lakini ilizikataa hoja nyingine ambazo zingeweza kusababisha rufaa hiyo kutupwa kama iungezikubali, hivyo ikaamua kuendelea na usukilizwaji wa rufaa hiyo.

Hata hivyo muda wa usikilizwaji wa rufaa hiyo ulipofika, ndipo mawakili wa Serikali wakaiarifu mahakama kuwa wamewasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo wa Mahakama Kuu.