Chadema waja na hoja tatu kuhusu kauli ya Lugola

Mkurugenzi wa operesheni na mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila 

Muktasari:

Leo Alhamisi Februari 14, 2019, Chadema wamemjibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye jana amemtaka, Tundu Lissu kurejea Tanzania kusaidia upelelezi wa tukio lake la kushambuliwa na risasi


Dar es Salaam. Leo Alhamisi Februari 14, 2019, Chadema wamemjibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ambaye jana amemtaka, Tundu Lissu kurejea Tanzania kusaidia upelelezi wa tukio lake la kushambuliwa na risasi.

Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 nje ya nyumba aliyokuwa akiishi jijini Dodoma Septemba 7, 2017 na jana Lugola katika mkutano wake na wanahabari jijini Arusha, alimtaka mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema), kurejea nchini kwa kuwa yeye na dereva wake ni mashahidi muhimu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam mkurugenzi wa operesheni na mafunzo wa Chadema, Benson Kigaila amesema chama hicho kimepokea kwa masikitiko kauli ya Lugola.

Amesema wanaotakiwa kufanya uchunguzi na kutoa majibu ya suala hilo ni Jeshi la Polisi.

Kigaila amesema kazi ya kukamata, kuchunguza na kufikisha mahakamani ni ya Serikali na kwamba Lugola alitakiwa kuwaeleza Watanzania nini Serikali imekifanya kuchunguza tukio hilo.

"Atuambie (Lugola) anamtaka Lissu arudi kwa document (nyaraka) gani ya kiofisi au anataka tuanze kufanyia kazi mambo ya mtaani,” amehoji.

Kigaila amesema kwa mujibu wa maelezo ya Lugola, Serikali haiwezi kuchunguza tukio ambalo mhusika yupo nje ya nchi, akibainisha kuwa kuna matukio mengi yamewahi kuchunguzwa wakati wahusika wakiwa hawapo.

"Wakati Lissu anapigwa risasi hao walinzi wa kampuni binafsi walikuwa wapi? Lugola awaeleze Watanzania hao anaowaita walinzi binafsi wanaolinda nyumba hizo walichukua hatua gani? Hao ndio walitakiwa kuwa wa kwanza kueleza,” amesema.