VIDEO: Chadema wamkingia kifua Sugu, watoa ujumbe kwa polisi

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salumu Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar kulaani. Mbuge wa  Mbeya Mjini kuhojiwa na Jeshi la Polisi kuhusu maradi wa vitambulisho vya wamachinga. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Chadema watoa msimamo kuhojiwa kwa Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ wataka watendaji jeshi la polisi wajitathmini na kutojiingiza kwenye siasa

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania kimewataka watendaji ndani ya Jeshi la Polisi kujitathmini na kuzingatia weledi katika utekelezaji wa majukumu yao.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Februari 22,2019 makao makuu ya chama hicho Kinondoni jijini Dar es Salaam, amesema kuna baadhi ya watendaji wa jeshi hilo wamekuwa wakisukumwa na mihemko ya kisiasa na matokeo yake wanawaonea wapinzani.

Kauli hiyo ya Mwalimu imekuja kufuatia kitendo cha jana Alhamisi cha jeshi la polisi Mbeya kumhoji mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema) Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kwa kuwakusanya watu na kuhoji suala la vitambulisho vya wamachinga.

“Tunaposema nchi haina haki, usawa wala demokrasia mambo ni kama haya yanaonekana hadharani. Mpinzani akizungumza na wananchi wake ni kosa ila viongozi wa CCM wanazunguka nchi nzima hakuna anayewauliza,” amesema Mwalimu.

“Watendaji ndani ya jeshi la polisi wajitathmini, wajiangalie waachane na mambo ya siasa watalipeleka pabaya taifa. Polisi watimize jukumu lao la kulinda usalama na kuzingatia weledi,” ameongeza.

Amesema chama hicho hakikubaliani na kitendo alichofanyiwa Sugu na kinataka aachwe afanye kazi zake na kutekeleza majukumu yake kama mbunge wa Mbeya kwa uhuru.

Kwa mujibu wa Mwalimu anachofanyiwa Sugu ni wivu kwa sababu anapendwa na kukubalika zaidi na wakazi wa Mbeya mjini.