Chadema wataka polisi kumhoji Dk Mollel shambulio la Lissu

Monday February 11 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Polisi wakieleza kutofahamu chochote juu ya madai ya mbunge wa Siha (CCM), Dk Godwin Mollel kuihusisha Chadema na tukio la kushambuliwa kwa Tundu Lissu, chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimesema kitalishangaa jeshi hilo kama halitamhoji mbunge huyo.

Ijumaa iliyopita, Dk Mollel akichangia bungeni taarifa ya mwaka 2018 ya kamati za katiba na sheria na ile ya sheria ndogo alisema Chadema kupitia vikosi vyake vya kigaidi ndiyo iliyompiga risasi Lissu na kwamba kuna wafadhili wake nje ya nchi ambao wanaipatia fedha kuratibu shughuli za vikosi hivyo.

Hata hivyo, alipoulizwa jana kuhusiana na madai hayo ya Dk Mollel, msemaji wa Jeshi la Polisi, Ahmed Msangi alisema hajasikia chochote kuhusu kauli hiyo hivyo hawezi kuizungumzia.

Lakini wakati Msangi akisema hayp, mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na nambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema ushahidi wa Dk Mollel haupaswi kuachwa ukapotea.

Alisema Jeshi la Polisi linapaswa kutumia kauli ya mbunge huyo wa Siha kama sehemu ya kuanzia ili wafungue upya jalada la uchunguzi wa tukio hilo la Lissu.

Kuhusu vikundi vya ugaidi, Mrema alisema, “Ni vyema pia angepeleka ushahidi polisi ili suala hilo lishughulikiwe maana ugaidi ni kitu serious (kizito).”

Mrema aliwataka wabunge wa CCM waliokuwa Chadema kuacha kutunga habari za uongo kuhusu chama hicho ili waaminike walikohamia kwani hilo halitabadilisha ukweli kwamba wao ni mamluki.

Madai ya Dk Mollel

Dk Mollel aliyekuwa mbunge wa Chadema katika jimbo hilohilo kabla ya kujiuzulu na kujiunga na CCM mwaka jana, aliendelea kujenga hoja akikihusisha chama hicho na shambulio la Lissu akisema ndio maana viongozi wake waligoma kupeleka Afrika Kusini sampuli ya uchunguzi wa tukio la mlipuko wa mabomu yaliyotokea jijini Arusha, baada ya yeye kuziiba katika uchunguzi.

“Nikawaeleza kuna vitu nimeviiba na nikasema ninavipeleka kwa mkemia mkuu Afrika Kusini walikataa, waseme kwa nini walikataa,” alisema Dk Mollel.

“Wanapinga suala la Tundu Lissu? Chacha Wangwe (marehemu) kilimtokea nini baada ya kutaka uenyekiti (wa Chadema)? Kulikuwa na mpango namba moja wa kuzuia Serikali isifanye kazi na katikati ya mpango huo Lissu akapigwa risasi ili kusisimua watu wavuruge Serikali yetu,” alisema.

“Mpango namba mbili ndio unaendelea Ulaya ambao ni mwendelezo wa kufadhiliwa na watu wachafu ambao ni wezi wa rasilimali za kidunia… hakuna rasilimali ya Tanzania ambayo itakwenda nje wakati Watanzania wapo. Tanzania haiuzwi kwa makubaliano ya nyinyi kufika Ikulu,” alisema.

Akifafanua zaidi alichokisema bungeni wakati akizungumza na Mwananchi juzi, Dk Mollel alisema anafahamu kuhusu vikosi hivyo na yuko tayari kuzungumzia hata nje ya Bunge kwa kuwa ana ushahidi wa hilo.

“Ninaweza kuthibitisha na ndio maana ninaweza kusema popote wanipeleke mahakamani, fedha wanazozipata wanatumia kufadhili vikundi hivyo,” alisema mbunge huyo ambaye kitaaluma ni daktari wa binadamu.

Alisema anafahamu kuwapo kwa mpango wa vikosi hivyo kutumika kumuangamiza ila anajua havina uwezo huo.

“Nawaambia huo mpango wao hautafanikiwa, kwa vikosi hivyo ambavyo vinampiga mtu risasi kibao hawana uwezo wa kunidhuru na wala wasijaribu,” alidai.

Mbunge huyo alisema ana mpango wa kuishtaki Chadema kwa kukiuka haki za Lissu kwa kumzungusha katika mataifa mbalimbali ilhali akiwa bado mgonjwa.

Kuhusu tukio la Lissu

Lissu alishambuliwa mchana wa Septemba 7, 2017 akiwa ndani ya gari, nje ya makazi yake Area D, mjini Dodoma wakati akitoka kuhudhuria mkutano wa Bunge. Alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya.

Alipata matibabu katika hospitali hiyo hadi Januari 6, mwaka jana alipohamishiwa Ubelgiji.

Tangu Septemba 7, 2017 hadi Desemba 31, 2018, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema ametibiwa kwa siku 480 sawa na mwaka mmoja, miezi mitatu na siku 24 na hivi sasa anaendelea na matibabu licha ya kuruhusiwa kutoka hospitali na yupo katika ziara aliyoianza Ulaya na sasa Marekani akieleza kuhusu shambulio hilo na masuala mbalimbali ya demokrasia na utawala bora kuhusu Tanzania.

Advertisement