Chadema yasikitika kumkosa Maalim Seif, kumpa ushirikiano

Muktasari:

 

  • Mwaka jana Baraza la Wazee la Chadema lilitangaza kumkaribisha Maalim Seif kujiunga na chama hicho kikuu cha upinzani wakati mgogoro wa CUF ukizidi kukua, hata hivyo katibu mkuu huyo wa zamani wa CUF ameamua kujiunga na chama cha ACT-Wazalendo.

Dar es Salaam. Chadema imesema ilitamani kumchukua aliyekuwa katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, lakini hawakufikia makubaliano, hata hivyo wameamua kushirikiana naye katika chama chake kipya cha ACT Wazalendo.

Maalim Seif alikuwa mmoja wa wanasiasa waliounga mkono kwa nguvu zote uamuzi wa vyama vinne vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumuunga mkono Edward Lowassa aliyeteuliwa na Chadema kugombea urais.

Msimamo wake ndio uliomfanya mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujivua uanachama, lakini akarejea takriban miezi nane baadaye akitaka arejeshewe madaraka, hali iliyoibua mgogoro ulioishia mahakamani na baadaye Maalim Seif na wafuasi wake kushindwa kesi na kuamua kujiondoa na kujiunga ACT Wazalendo ambayo haikuwamo Ukawa wala haikumuunga mkono Lowassa uchaguzi mkuu uliopita.

Siku moja baada ya Maalim Seif na wenzake kupokelewa ACT –Wazalendo, Chadema kimeweka bayana yaliyojiri kati yake na mwanasiasa huyo mkongwe nchini.

Akizungumza leo jijini Dar es salaam, naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum  Mwalimu amesema licha ya kumkosa Maalim Seif na kundi lake wataendelea kushirikiana naye kwa kuzingatia mkutano wa vyama vya upinzani uliofanyika Zanzibar Desemba 2018.

"Hakuna pigo, tulimtaka kweli. Viongozi wetu kwa hekima na busara waliona huyu mtu akija huku ni jambo jema na sisi tuliona tunusuru hadhi na heshima yake na mapambano ya demokrasia."

"Sasa kama amekwenda kwa mwenzio, ndugu yangu hajaolewa binti yako ameolewa binti wa baba mdogo, sasa si mulemule?"

"Kama ni tajiri utashindwa kwenda kuomba chakula? Maana una binti  na mdogo wako ana binti, hajaolewa wako kaolewa wa ndugu yako, hayo si mule mule? Hutahudhuria sherehe?" amehoji.

Mwishoni mwa mwaka jana, Baraza la Wazee la Chadema lilitoa tamko la kumkaribisha Maalim Seif kwenye chama hicho wakati mgogoro wa CUF ukirindima.

Kuhusu nguvu ya Chadema Zanzibar, Mwalimu amesema chama hicho kitaendelea na programu zake, lakini hakitapambana na ACT-Wazalendo.

"Kuimarika kwa Chadema Zanzibar haimaanishi kukwamisha wale wanaoweza kusaidia mission ya mageuzi kule. Tunapambana ili tumsaidie yule na kumuimarisha yule mwenye nguvu. Kama itatokea na sisi tuna nguvu zaidi ni imani yetu watatokea wengine kuimarisha nguvu na si kutudhoofisha," amesema.

Alisema wataendelea na maazimio ya ushirikiano na vyama sita vilivyokutana Zanzibar mwaka jana.