Chama cha wazee chakerwa kuzagaa kwa ombaomba mitaani

Friday December 19 2014

By Anthony Kayanda, Mwananchi

Kigoma. Serikali imetakiwa kuwaondoa kwa nguvu ombaomba wote mitaani kwani kuwaacha ni kuwadhalilisha na kudumaza maendeleo ya familia zao, ikiwa ni pamoja na kujenga hisia kwa watoto kuwa kuomba mitaani ni mojawapo ya ajira sahihi.

Akizungumza mjini hapa juzi, Katibu wa Chama cha Saidia Wazee Tanzania (Sawata) Tawi la Kasulu, mkoani Kigoma, Clotilda Kokupima alisema kuwapa fedha ombaomba hao siyo suluhisho la kuwakomboa na umaskini unaowakabili.

Kokupima alisema kitendo cha wazee kuongozana na watoto au wajukuu zao kuomba mitaani ni jambo lisilofaa na linatakiwa kulaaniwa kwa sababu linajenga misingi mibovu ya kujitegemea.

“Serikali iwaondoe hawa watu wote mitaani, utashangaa siku ya Ijumaa ombaomba wanajazana kwenye maduka na maeneo mengine kuomba. Hata sisi tunaowapa fedha tunatoa Sh50 au Sh100, sasa hizi zitawasaidia nini, naomba Serikali iwape mafunzo ili wajitambue na wapange mikakati yao ili wajitegemee,” alisema Kokupima.

Hata hivyo, Kokupima alisema baadhi ya wazee wanaishi katika mazingira magumu ya kuokota mabaki ya vyakula kwenye mapipa ya takataka, huku wengine wakipewa mabaki ya vyakula na majirani zao.

Alisema hali hiyo inaonyesha ni kwa jinsi gani wazee hao wanavyohitaji msaada mkubwa kutoka serikalini na kwa wadau wengine.

“Mbali ya kukosa chakula, hawana mavazi, utamkuta babu kavaa kaptula aliyoitengeneza kwa kutumia gunia yuko mtaani, inasikitisha,” alisema.

na wanawake wanavaakanga moja ambayo huitumia kama shuka usiku wakiwa na wajukuu zao waliotelekezwa na Wazazi wao, hawa watu wanahitaji msaada wasiachwe wakiranda barabarani,” alisema.

Sawata imeshaanzisha mchakato wa kuwatambua wazee wote wasiojiweza wilayani Kasulu.

Baadhi ya wazee waliozungumza na gazeti hili ambao hawakutaka majina yao yatawe gazetini, walisema hali ngumu ya maisha ndiyo inayowasukuma kuingia mitaani kuomba misaada.

Advertisement