Changamoto mabasi ya mwendokasi mwisho Agosti

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo akipata maelezo kutoka kwa mhandisi wa Manispaa ya Temeke kuhusu ujenzi wa barabara zilizopo kwenye mradi wa DMDP, Allen Mshiu ya ujenzi awamu ya pili kutoka Kariakoo kwenda Mbagala jijini Dar es Salaam jana. Picha na Salim Shao

Muktasari:

  • Baada ya changamoto za muda sasa katika usafiri wa mabasi yaendayo haraka, Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo amesema mpaka Agosti mwaka huu watumiaji wa usafiri huo watakuwa na furaha kama zamani.

Dar es Salaam. Waziri wa nchi ofisi ya Rais, Tamisemi, Suleiman Jafo amesema changamoto zote zilizopo katika mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart) zitakuwa zimetatuliwa hivyo wakazi wa jiji la Dar es Salaam wataanza kufurahia upya usafiri huo.

Jafo amesema hayo leo Jumamosi Aprili 20, 2019 wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa vituo vidogo vya mabasi yaendayo haraka ambavyo ni sehemu ya awamu ya pili ya Dart kutoka Gerezani hadi Mbagala.

"Tatizo kubwa ni uchache wa mabasi, mtoa huduma wa muda (Udart) alipaswa kuwa na mabasi 305 kwa ajili ya awamu ya kwanza lakini yeye alilete mabasi 140 na yote hayawezi kufanya kazi kwa pamoja, abiria wanaotumia mwendokasi kwa siku wanakadiriwa kuwa 370,000 hivyo lazima kuwe na shida," amesema.

Amesema tayari tangazo la kumtafuta mtoa huduma mpya limetolewa Aprili 17 mwaka huu hivyo mpaka Agosti mwaka huu  changamoto hiyo itakuwa imetatuliwa.

Jafo amesema mabasi 70 yaliyokwama bandarini ambayo yalikuwa yameagizwa na Udart yana issue nyingine za mapato na Dart (Wakala wa Serikali wa mabasi yaendayo haraka) haihusiki nayo lakini Udart wakimalizana na TRA wanaweza kuzungumza na Dart kuona cha kufanya kwa kuwa hakuna jambo lisilowezekana.

"Awamu ya kwanza ya mradi huu tumetupa fundisho kubwa kutokana na changamoto zake, Watanzania wanapaswa kufurahi kwa kupata mradi huu awamu zinazofuata zitakuwa bora kwa kuwa tumeshapata somo," amesema Jafo.

Aidha katika matembezi hayo ya waziri katika vituo vinnee (Duce, Kijichi, Zakiemu na Mbagala) mkandarasi amelalamika kutopatiwa umeme licha ya kulipa gharama zote mapema na Jafo alimuahidi kuwa ataongea na waziri wa nishati ili kutatua changamoto hiyo ili isije kuwa sababu ya kuchelewa kwa mradi huo," amesema Jafo.

"Tuna changamoto, hatujapata umeme wala maji lakini sasa mradi umekamilila kwa asilimia 6 ikiwa ni mwezi mmoja tangu tulipoanza na tuna imani tutakamilisha kwa muda kwani mkataba wetu ni miezi 24," amesema Kaiza Joseph ambaye ni mhandisi wa Kampuni ya CCECC ambayo inatekeleza kandarasi hiyo kwa Sh44.8 bilioni.

Meneja wa kampuni Inter Consult ambayo ndiyo mshauri katika mradi huo, Benny Matata amemhakikishia waziri kuwa kampuni yake itamsimamia mkandarasi kuhakikisha mradi unafanyika kwa ubora na kukamilika kwa muda uliopangwa.