Chenge, Dk Kijaji ‘wapambana’ na Mnyika matumizi ya Sh976 bilioni

Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge akiwaonyesha wabunge vitabu vya ukaguzi vya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2018, alipokuwa akiongoza kikao cha tisa cha mkutano wa Bunge la Bajeti, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika ameitaka Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kutoa majibu ya matumizi ya Sh976.96bilioni.

Dodoma. Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge amelazimika kuomba kumbukumbu rasmi za bunge (Hansard) ili kufuatilia na kutoa majibu ya hoja ya Mbunge wa Kibamba (Chadema), John Mnyika aliyeitaka ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kueleza matumizi ya Sh976.96 bilioni.

Amechukua uamuzi huo leo kutokana na mbunge huyo kuibua sakata hilo huko akikumbushia sintofahamu ya matumizi ya Sh1.5 trilioni yaliyoibuliwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad katika ripoti ya ukaguzi ya mwaka 2016/17.

Mbunge wa Kibamba, John Mnyika akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Mnyika alikuwa akijadili bajeti ya Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Utata wa matumizi ya Sh1.5 trilioni uliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe wakati akichambua ripoti ya CAG.

Tangu suala hilo lilipoibuliwa Aprili mwaka jana kumekuwa na mijadala mara kadhaa ndani na nje ya Bunge hasa kutoka kwa upinzani uliokuwa ukitaka maelezo ya kuwapo kwa tofauti ya uwiano wa mapato na matumizi ya kiasi hicho cha fedha ambacho Zitto alidai hakionekani jinsi kilivyotumika katika ripoti ya CAG.

“Nitaomba kupata ufafanuzi kutoka ofisi ya Rais, ripoti iliyopita ya CAG iliibua madudu mengi katika sekta na wizara mbalimbali na  kati ya mambo yaliyoibuliwa ni pamoja na Sh1.5 trilioni na kupanda hadi 2.4 trilioni.”

“Katika ufafanuzi wa Serikali kuna taarifa zilitolewa kwamba Sh976.96 bilioni zilihamishwa kwenye mafungu mbalimbali zikapelekwa kwenye fungu la 20 la bajeti ambalo ni sehemu ya hotuba yetu ya leo ya ofisi ya Rais Ikulu.”

 “Kama mbunge naamini Bunge halikupitisha  uamuzi wa kuhamisha fedha hizo kupeleka Ikulu,” amesema Mnyika.

Baada ya kauli hiyo, Chenge aliingilia kati, “Hebu nisaidie sheria ya bajeti kuhusu kuhamisha fedha inasemaje, ni Bunge linafanya au mamlaka husika.”

Katika majibu yake Mnyika amesema: “Kwa ajili ya muda naomba nijikite katika hoja yangu tukitaka kulijadili hilo tutachukua muda.”

Chenge alizidi kumbana Mnyika akimtaka kutojumuisha mambo ambayo hawezi kuyatolea majibu.

“Sisi  wote tumeshiriki katika utungaji wa sheria hiyo (ya bajeti), kiwango kilichotajwa na sheria ya bajet kama kuna mbunge anatakiwa kupinga hilo, uhamishaji wa fedha ukiwekwa na Serikali hapa wewe (mbunge) unatakiwa useme uhamishaji huo unazidi kiwango kilichowekwa na Bunge (ukomo) lakini hatuwezi kufanya majumuisho tu,” amesema.

Alipotakiwa kujibu Mnyika amesema, “Ili tuondoe utata kuhusu jambo hili la Sh Sh976.96 bilioni, kwa kuwa CAG anabanwa kukagua Ikulu ofisi ya Rais wakiwa wanajibu (hoja za wabunge) watueleze hizi fedha zimetumikaje?"

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji akiomba muongozo wa Mwenyekiti Wabunge alipokuwa akitaka Mbunge wa Kibamba, John Mnyika afute baadhi ya kauli zake alizozitoa wakati akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashantu Kijaji naye alitolea ufafanuzi hoja ya Mnyika akibainisha kuwa ni lazima suala hilo lijibiwe leo na si siku ambayo mawaziri kwa pamoja watajibu hoja zote za wawakilishi hao wa wananchi walizozitoa wakati wakichangia bajeti hiyo.

“Mnyika athibitishe kwamba CAG anabanwa kukagua fungu 20 la ofisi ya Rais kwa sababu kinachofahamika kila fungu lina resident auditor kutoka ofisi ya CAG likiwamo fungu 20.”

“Hakuna fungu hata moja ambalo CAG anazuiwa kukagua na fungu hili lilikaguliwa, hoja zake (Mnyika) anawadanganya Watanzania, anamchafua Rais bila sababu za msingi,” amesema Dk Kijaji.

Alipotakiwa kuendelea kuchangia Mnyika amesisitiza, “Naomba katika majumuisho ofisi ya Rais ilete mchanganuo hizi fedha zimetumika kwenye kitu gani.”

Mbunge wa Uranga (CCM), Goodluck Mlinga (CCM) aliomba kuhusu utaratibu  akitumia kanunia ya 64 (a) ya Bunge.

“Suala la Sh1.5trilioni limeendelea kuzungumzwa bungeni kwa uongo, ripoti ya PAC (Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali) ambayo mwenyekiti wake ni mpinzani (Naghenjwa Kaboyoka) wa Chadema  katika ukurasa wa 35 inasema kuwa tofauti ya Sh1.5trilioni haikuwapo baada ya mahesabu kurekebishwa.”

“ Ila hili suala limeendelea kuzungumzwa na Bunge linakaa kimya, suala hili likemewe na (Chenge) utoe maelekezo.”

Katika ufafanuzi wake Chenge amesema: “Kwa  mujibu wa kanuni zetu kwa sababu ya uamuzi wa  kamati ya PAC kwa hayo uliyoyasema unatakiwa kuthibitisha ni kweli au si kweli, kwanza kufuta kauli yako kuhusu Sh2.4 trilioni kwa maana kwamba 1.5 trilioni kujumlisha hizi bilioni.”

“Maelezo ya Sh1.5 trilioni yapo katika ripoti ya CAG, sasa futa kauli yako au uthibitishe hapa bungeni, nikupe muda uthibitishe, chagua moja,” amesema Chenge.

Mnyika amesema, “Naomba kuweka rekodi sawa, nimesema nataka maelezo ya Serikali bungeni juu ya Sh 976.96 bilioni zimetumika kwa matumizi gani na hii ndio inasababisha mjadala wa Sh 1.5trilioni na Sh 2.4trilioni kuendelea. Kama ni uthibitisho basi ni Sh 976.96 bilioni za fungu 20 za Ikulu.”

Kutokana na Mnyika kuendelea kushikilia hoja yake, Chenge alisema mbunge huyo ni kama anawapotezea muda na kuagiza kupata taarifa za kumbukumbu za Bunge ili kufuatilia vyema hoja yake na kutoa uamuzi  leo saa 7:00 mchana kabla ya kuahirishwa kikao hadi saa 11:00 jioni.

Hata hivyo, ilipofika muda huo Chenge aliahirisha kikao hicho bila kutoa ufafanuzi wa hoja hiyo.