Cheti cha kuzaliwa kupatikana kiulaini

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) Emmy Hudson

Muktasari:

  • Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo mikoa ya Singida na Dodoma, alisema usajili huo unafanyika kwenye ngazi za chini ambako kila mtoto anayezaliwa anaandikishwa bila usumbufu wowote na vyeti vinatolewa wakati huohuo na bila malipo.

Singida. Ilikuwa jambo la kawaida kusafiri hadi zilipo ofisi za wakuu wa wilaya kufuatilia vyeti vya kuzaliwa na wakati mwingine usipate haraka.

Umbali huo kutoka kwenye makazi ya watu mpaka vituo vya usajili ndio uliosababisha asilimia 13.4 pekee ya Watanzania kuwa na vyeti hivyo kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya 2012. Lakini kupitia mpango wa kusajili watoto chini ya miaka mitano unaofanyika katika mikoa 13 nchini, vyeti hivyo vinapatikana kwa muda mfupi katika zahanati za vijiji, vituo vya afya na ofisi za kata.

Kaimu mkurugenzi mtendaji wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) Emmy Hudson alisema juzi kuwa tayari watoto milioni tatu wameshasajiliwa.

Akizungumza katika uzinduzi wa mpango huo mikoa ya Singida na Dodoma, alisema usajili huo unafanyika kwenye ngazi za chini ambako kila mtoto anayezaliwa anaandikishwa bila usumbufu wowote na vyeti vinatolewa wakati huohuo na bila malipo.

Alisema vyeti hivyo tayari vimeshachapwa na uandikishaji wake hauhitaji mashine wala umeme isipokuwa kujazwa kwa kalamu ya wino katika maeneo muhimu.

Hudson alisema baada ya mtoto kusajiliwa, moja kwa moja taarifa zake zinatumwa kwenye kanzidata kupitia simu ya mkononi.

Mkuu wa Wilaya ya Singida, Pascas Muragili alisema mpango huo utamaliza msongamano kwenye ofisi za wakuu wa wilaya kusaka vyeti.

Mwakilishi mkazi wa Unicef nchini, Maniza Zaman alisema ni haki ya kila mtoto kusajiliwa katika nchi yake na wao wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha wanaozaliwa wanaandikishwa.

Akizindua mpango huo, Waziri wa Katiba na Sheria, Augustine Mahiga alisema usajili wa vizazi husaidia kupata takwimu sahihi za idadi ya watu kwa ajili ya maendeleo na kuepuka matumizi ya takwimu za makisio.