China yaipa Bunge la Tanzania kompyuta mpakato 70

Spika wa Bunge, Job Ndugai akipokea msaada wa komputa mpakato kutoka kwa Balozi wa China nchini, Wang Ke katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika Bungeni, jijini Dodoma leo. Bunge limekabidhiwa msaada wa komputa mpakato 70 kwa ajili ya kuwawezesha kufanya kazi vizuri na kupunguza matumizi ya karatasi. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Bunge la Tanzania limepokea kompyuta mpakato 70 ikiwa ni msaada kutoka China, ambazo zitagawiwa kwa baadhi ya wabunge wa Bunge  hilo 392.

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema makabrasha wanayopewa wabunge katika kipindi hiki cha Bunge la Bajeti, yanaweza kujaa gari ndogo aina ya pickup kwa kila mbunge hivyo wanalenga kusafisha meza za wabunge.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo leo Jumanne Juni 26,2019 wakati akitoa maelezo ya msaada wa kompyuta mpakato 70 ambazo zimetolewa na Serikali ya China na kukabidhiwa na Balozi wa nchi hiyo, Wang Ke.

Amesema wabunge hupewa makabrasha mengi ambayo wakati mwingine yanakuwa yamechafua meza zao na pia ni mzigo wakati wa kurudi makwao hivyo wanashindwa kubeba na wakifika makwao wanakosa rejea.

“Tumepewa hizi kompyuta mpakato lakini lengo letu ni kila mbunge kuwa na kompyuta ili taarifa zitumwe humo na waweze kutembea nazo kila wanakokwenda badala ya utaratibu huu wanashindwa kufanya rejea,” amesema Ndugai.

Naibu Spika wa Bunge hilo,  Dk Tulia Akson amesema bado kuna kazi ya kuwasaidia kupata elimu kwa kuwa baadhi ya wabunge hawajawa na ujuzi wa kutumia kompyuta.

Dk Tulia amesema kwa idadi ya kompyuta zilizotolewa na China ni ndogo lakini watakaa na kuona namna ya kuzigawa kwa wabunge wachache wakati Bunge linaendelea kujipanga kuongeza zingine.

Awali, Balozi Wang Ke amesema ushirikiano uliopo baina ya China na Tanzania utaendelea kudumishwa na nchi hiyo haitasita kuisaidia Tanzania inapobidi.

Balozi Ke amesema msaada huo unatokana na ziara ya Naibu Spika wa Bunge la China alipotembelea Bunge la Tanzania mwaka 2018 ambapo aliahidi kutoa msaada wa vitendea kazi hivyo.