Congo yaomba kujiunga Jumuiya ya Afrika Mashariki

Muktasari:

Katika kuendelea kuimarisha uhusiano baina yake na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais wa Congo Tshisekedi amesema wameshaomba kujiunga na EAC.


Dar es Salaam. Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi amesema nchi hiyo tayari imeshaomba kujiunga na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais Tshisekedi amesema hayo leo Ijumaa June 14, baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam wakati wa ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Tanzania.

Amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili na kwamba namna nzuri zaidi ya kuendelea kuimarisha mahusiano hayo ni kupitia ujenzi wa miundombinu.

“Bila shaka miundombinu hii itasaidia kuongeza biashara kati ya wananchi wetu na kwa wasiofahamu Congo tayari imeomba kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwani itakuwa jumuiya muhimu sana duniani,” amesema Rais wa Congo, Tshisekedi

Kiongozi huyo wa Congo amesema ili kufikia katika hatua hiyo lazima kuendeleza miundombinu na ushirikiano ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

Aidha amesema yapo mengi ya kujifunza kutokana na utendaji kazi wa viongozi wa Tanzania, hasa Rais John Magufuli katika kuimarisha uchumi.

“Rais anaonyesha mfano mzuri sana hata sisi kule Congo tutachukua mfano huu kuiga yale mazuri anayofanya,” amesema.

Awali Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwele  amesema bandari ya Dar es Salaam ndiyo iliyo rahisi kutumiwa na wafanyabishara wa nchi jirani ikiwa Jamuhuri ya Kidemoktasia ya Congo.

Hata hivyo, nchi za DRC, Rwanda, Zambia, Burundi zimekuwa zikutumia bandari hiyo japo kwa kipindi cha karibuni mizigo ya nchi hizo ilikuwa imepungua.