DC Jokate aonya matumizi ya mtandao

Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Jokate Mwegelo, akizungumza wakati wa Mdahalo ulioandaliwa na Plan International jijini Dar es Salaam leo kuhusu namna ya usawa wa kijinsia unavyoweza kuleta maendeleo

Muktasari:

Mkuu  Wilaya ya Kisarawe,  Jokate Mwegelo amewataka vijana kutotumia mitandao ya kijamii kusambaza umbea badala yake waifanye kama nyenzo ya mafanikio yao kiuchumi.

Dar es Salaam. Mkuu  Wilaya ya Kisarawe,  Jokate Mwegelo amewataka vijana kutotumia mitandao ya kijamii kusambaza umbea badala yake waifanye kama nyenzo ya mafanikio yao kiuchumi.

Amesema huenda mitandao hiyo ilifika wakati wengi wakiwa bado hawajajiandaa lakini matumizi sahihi ya nyenzo hiyo yanaweza kuwafikisha mbali kiuchumi.

Akizungumza leo Jumatano Mei 15, 2019 katika mdahalo ulioandaliwa na Plan International  kuhusu namna usawa wa kijinsia unayoweza kuchochea maendeleo,  Jokate amesema vijana wanaweza kushikamana kwenye masuala ya msingi yanayoweza kuibadilisha jamii kifikra kupitia mitandao.

"Mitandao ya kijamii ni kama kisu, ukichinja kuku utakula na kufurahi lakini ukikitumia vibaya utamjeruhi mtu na hata kumuua halafu utapata kesi, kwa hiyo mitandao ya kijamii ni nyenzo tukitumia vizuri,"  amesema  Jokate.

"Nimeona dunia ya pili ya mitandao kwa sababu vijana wengi wameunga mkono  kampeni hii na inaendelea vizuri," amesema Jokate.

Amewataka wasichana kuamua kwamba ikiwa watasoma kwa bidii na kuepuka vishawishi wanaweza kufikia ndoto zao.