DC Kigamboni amzungumzia mwanamke aliyeuawa kisha kuchomwa moto

Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Sara Msafiri akizungumza na wakazi wa kata ya Somangila kufuatia tukio la mauaji ya Naomi Marijani

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutoa taarifa wanapoona hali isiyo ya kawaida kwa wenzao bila kujali kuwa wataonekana wanaingilia masuala ya familia

Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sara Msafiri amewataka wakazi wa wilaya hiyo kutoa taarifa wanapoona hali isiyo ya kawaida kwa wenzao bila kujali kuwa wataonekana wanaingilia masuala ya familia.

Sara ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Julai 19, 2019 katika mkutano wa hadhara na wakazi wa Kigamboni, kugusia tukio la Naomi Marijani aliyeuawa na kuchomwa moto na mumewe, Khamis Luwongo.

Kamanda wa Polisi wa Temeke, Amon Kakwale amesema juzi kuwa mume huyo, amekiri kumuua mkewe anayeitwa na baadaye kuchimba shimo kwenye banda la kuku ambalo alilitumia kumchoma kwa moto wa magunia mawili ya mkaa na kisha kwenda kufukia majivu shambani.

Kwa mujibu wa polisi, baadaye mumewe alikwenda polisi kutaarifu kuwa Naomi amepotea. Naomi alitoweka nyumbani Mei 15, 2019.

Pamoja na polisi kusema mume huyo amekiri kumuua mkewe, familia italazimika kusubiri takriban siku 10 kuthibitisha kama majivu yaliyopelekwa kufanyiwa kipimo cha vinasaba (DNA) ni ya ndugu yao.

Katika mkutano huo,  Sara amesema wananchi wakijenga tabia hiyo itasaidia kunusuru maisha ya watu walio hatarini ili yasiwakute kama yaliyomkuta Naomi.

“Nina uhakika  hadi huyu bwana anafanya hivi lazima kuna shida sehemu na watu wa karibu mnafahamu  ila mkaona hayawahusu, hii ni hatari.”

“Tunapokaa huko wanawake tunahadithiana shida kwenye ndoa zetu, lakini tunaishia kuzikumbatia hatusaidiani matokeo yake yanafikia hatua hii kama yaliyomkuta Naomi,” amesema Sara.

Mkuu huyo wa wilaya amesema ameshangazwa na kitendo cha kukosekana kwa jirani aliyebaini kuchomwa moto kwa Naomi wakati nyumba aliyokuwa anaishi imezungukwa na nyumba nyingi.

“Binadamu akichomwa lazima ingesikika harufu ya nyama na huo moshi ulipita wapi kiasi kwamba wasione, gunia mbili za mkaa hadi zinateketea hakuna aliyehisi chochote au ndiyo kila mtu anajali maisha yake,” amehoji Sara.

Hata hivyo, amewahakikishia wananchi kuwa vyombo vya dola vitafanya kila linalowezekana ili sheria ichukue mkondo wake na haki itendeke.

Ameipongeza  familia ya Naomi kwa kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha zinakusanywa taarifa zilizofanikisha  kukamatwa kwa mtuhumiwa.