DC aliyemsweka rumande dereva wake, abadilishiwa dereva asema...

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya aviachia vyombo vya dola kuendelea na uchunguzi dhidi ya dereva wake pamoja na ofisi mmoja aliyempa fedha ili kumpelekea mkuu huyo wa wilaya ili kumwezesha kutembelea moja ya kiwanda wilayani humo

Hai. Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai ole Sabaya amesema ameviachia vyombo vya dola kuendelea na uchunguzi wa tukio la dereva wake, kutaka kumpa fedha kiasi cha Sh1 milioni alizopewa ili atembelee kiwanda kimoja (jina linahifadhiwa) wilayani Hai.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Machi 22,2019, Sabaya amesema kwa kuwa tayari suala hilo lipo polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ana imani watafanya uchunguzi wa kina ili kujua chanzo cha dereva huyo kupewa fedha kumpelekea ofisini.

"Mimi muda huu nipo vijijini, kushughulikia kero za wananchi, tayari nimepewa dereva mwingine na huyu hata kama akiachiwa simuhitaji tena kwani si msafi," amesema

Amesema anaamini vyombo husika vya uchunguzi, vikikamilisha kazi vitatoa taarifa ya kili kilichotokea hadi dereva huyo kupewa fedha aniletee ofisini ili nitembelee kiwanda jambo ambali sio sahihi.

"Mimi kama kiongozi wa umma ni wajibu wangu kutembelea miradi ya maendeleo na sipaswi kulipwa kwa kufanya kazi ambayo ni wajibu wangu, sasa watasema wenyewe hiyo fedha ni ya nini walitaka kunipa," amesema.

Katika hatua nyingine, Takukuru huenda ikatolea ufafanuzi wa tukio hili Jumatatu.

 Ofisa mmoja wa Takukuu ambaye aliomba kuhifadhiwa jina,  akizungumza na Mwananchi jana alisema suala hilo lipo katika uchunguzi na kama ukikamilika Jumatatu watatoa taarifa.