DC amsweka mahabusu dereva wake

Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya

Muktasari:

Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya amekataa kupokea Sh1 milioni alizopelekewa na dereva wake ambazo inadaiwa alipewa na mtu mmoja ili akatembelee kiwanda chake na kuagiza wakamatwe na vyombo vya dola viwachunguze

Moshi. Mkuu wa wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro, Lengai Ole Sabaya, ameamuru kukamatwa kwa dereva wake na mmiliki mmoja wa kiwanda wilayani humo kwa tuhuma za kutaka kumpa hongo ya Sh1 milioni.

Wawili hao walikamatwa juzi na kuswekwa mahabusu kituo cha polisi cha Bomang’ombe wilayani Hai na kwamba fedha hizo inadaiwa alipewa dereva wake huyo ili ampelekee ofisini.

Chanzo kimoja cha habari kimedai ingawa watuhumiwa hao wanashikiliwa kituoni hapo, wamekuwa wakitolewa na kwenda kuhojiwa na maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Ingawa kamanda wa Takukuru mkoa wa Kilimanjaro, Holle Makungu jana hakupatikana kuzungumzia suala hilo akisema yuko kwenye kikao nje ya mkoa, lakini Sabaya mwenyewe amethibitisha suala hilo.

“Ni kweli nimeagiza huyo dereva akamatwe ili uchunguzi ufanyike kujua ni kwa nini apewe Sh1 milioni ili aniletee ofisini ili nikatembelee kiwanda cha (jina limehifadhiwa). Hili ni kosa,” alisema.

“Mimi nadhani ni makosa, kwani mimi kama kiongozi wa Serikali ni wajibu wangu kutembelea viwanda na maeneo mengine yanayotoa huduma kwa jamii,” alisema Ole Sabaya.

Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hiyo alisema baada ya kupelekewa fedha hizo ofisini aliagiza vyombo vya usalama kumkamata na kufuatilia kiwanda hicho.

Sabaya pia ameagiza vyombo vya dola ikiwamo Takukuru kufutilia kiwanda hicho na ofisa aliyetoa fedha ili kujua lengo lao lilikuwa nini.

"Niwatake wakazi wa Hai wenye kero maeneo yao wakiwamo wafanyabiashara kufika ofisini kwangu na tutashirikiana na vyombo vingine vya Serikali kuwasaidia bila malipo yoyote," alisema.

Tukio la kiongozi wa Serikali mkoani Kilimanjaro kugoma kupokea fedha za aina hiyo si la kwanza, kwani Novemba 15 mwaka jana meneja wa TRA mkoa, Msafiri Mbibo alikataa kupokea kitita cha dola 2,000 za Marekani.

Rushwa hiyo inadaiwa ilitolewa na meneja wa fedha wa kampuni ya ujenzi wa barabara, Sureshbabu Kakolu ili ampe upendeleo na kupitisha maombi yake ya msamaha wa kodi inayofikia Sh6.6 bilioni.

Kakolu aliyekuwa meneja wa fedha katika kumpuni za Dott Services (TZ) Ltd na General Nile Company alikiri kosa hilo na kuhukumiwa kulipa faini ya Sh1 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela.

Mshitakiwa huyo alilipa faini hiyo na kuachiwa huru na tukio la Mbibo kukataa rushwa hiyo lilimgusa Rais John Magufuli na kumpongeza hadharani alipozungumza na wafanyabiashara jijini Dar es Salaam.