DC awakamata wanafunzi Igunga wakicheza kamari

Mkuu wa wilaya ya Igunga, John Mwaipopo

Muktasari:

Mwaipopo alimwamuru mkuu wa Shule ya Sekondari Igunga, kutoa adhabu ya viboko hadharani ambapo walichapwa vinne kila mmoja huku wananchi wakimpongeza mkuu wa wilaya kwa adhabu hiyo.

Tabora. Mkuu wa wilaya ya Igunga, John Mwaipopo ameamuru kutandikwa viboko hadharani wanafunzi sita wa sekondari baada ya kuwakuta wakicheza kamari muda wa masomo.

Wanafunzi walionaswa na mkuu huyo wa wilaya ni wa shule mbili za sekondari zilizopo kata ya Igunga ambao walicharazwa viboko vinne kila mmoja huku wengine wanne wakiwekwa mahabusu.

Akizungumza jana, Mwaipopo alisema akiwa katika ziara ya kugawa na kukagua vitambulisho vya wajasiliamali, mtaa wa Sokoni alikuta vijana 10 wakicheza kamari na alipowahoji sita walibainika ni wanafunzi wa sekondari. Alisema baada ya kuwakamata wanafunzi hao alimuita mkuu wa Shule ya Sekondari Igunga, Renatus Buswelu na kuwatambua watatu ni wa shule yake.

Alisema wanafunzi wengne watatu walibainika ni wa Sekondari ya Mwayunge na alimwita mkuu wa shule hiyo ambaye aliwatambua na kueleza wamekuwa watoro wa mara kwa mara.

Mwaipopo alimwamuru mkuu wa Shule ya Sekondari Igunga, kutoa adhabu ya viboko hadharani ambapo walichapwa vinne kila mmoja huku wananchi wakimpongeza mkuu wa wilaya kwa adhabu hiyo.

Vijana wengine wanne ambao si wanafunzi lakini walikuwa na wanafunzi hao walipelekwa kituo cha polisi Igunga.