DK Bashiru: ACT- Wazalendo siyo tishio kwa CCM

Friday April 26 2019

 

By Airea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Bashiru Ally amesema kuimarika kwa chama cha Act- Wazalendo hakuwatikisi kwa sababu bado NI kidogo kinachohitaji kujiimarisha.

Ameyasema hayo leo Aprili 26 katika kipindi cha Gumzo la Muungano kilichorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC 2) baada ya kuulizwa swali na muongozaji wa mahojiano hayo, Tido Mhando.

Dk Bashiru amesema chama hicho si tishio kwa CCM kwasababu kina na mwakilishi mmoja bungeni na kinaongoza halmashauri moja ya Kigoma Mjini, hivyo kuongezeka kwa wanachama huenda ikawa fursa kwao ya kuongeza wawakilishi.

Amesema kutoaminiana na mvurugano uliotokea ndani ya CUF na kufanya baadhi ya wanachama kuhamia Act Wazalendo ni jambo lililoleta shida kwao kwasababu ya kuhofia umoja wa kitaifa kuvurugika na kwamba CCM ipo tayari kufanya kazi na chama chochote.

“Hata ile shusha tanga pandisha tanga haikuwa na shida ila tu isiathiri umoja na wala amani. Maana hata sisi tulishtuka na hatukutarajia mabadiliko yale kwa sababu hatukuwahi chama kama kile kinaweza kuwa na mgogoro wa ndani unaoweza kusababisha mpasuko lakini tunamshukuru Mungu mambo yameenda salama.”

“Lakini hatukushtuka kwamba kunaenda kutengenezwa chama kitakachoitikisa CCM hapana, kwa sababu sisi hatupati tishio kutoka vyama vya siasa ila tunapata tishio baada kuona mgogoro ndani ya chama kwa sababu tunataka kushindana na vyama madhubuti,” amesema.

 Dk Bashiru amesema suala la umadhubuti wa vyama vya siasa hupimwa kwa kukubalika kwake kwa jamii na moja ya kipimo ni kushinda katika uchaguzi jambo ambalo CCM inajivunia.

Amesema kama chama kikishinda kwa asilimia zaidi ya 70 na kushikilia vijiji vingi lengo lake sio kudhoofisha vyama vingine bali ni kuonyesha jinsi gani kinakubalika.

“Kwa mfano tuangalie kiwango cha ushindi wa CCM tangu mwaka 1995 hadi sasa imekuwa ikifanya vizuri na vyama vingine vya siasa vimekuwa vikifanya hivyo katika baadhi ya maeneo hiyo ni kutokana na kukubalika kwake,” amesema Dk Bashiru.

Advertisement