DNA yaonyesha Sharon, Melon ni pacha

Nairobi, Kenya. Uchunguzi wa vinasaba (DNA) umebainisha wasichana Sharon Mathius na Melon Lutenyo ni pacha ambao mama yao halisi ni Rosemary Khaveleli Onyango.

Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mapacha hao na mama yao Rosemary wana chembechembe za kufanana kwa asilimia 99.999.

Mapacha hao ambao wamekuwa gumzo mitandaoni katika siku za karibuni katika nchi za Afrika Mashariki baada ya picha zao kuonekana hadharani wakionyesha kutoka katika familia mbili tofauti licha ya kufanana.

Lakini jana kitendawili cha wasichana hao wanaotoka kaunti ya Kakamega kiliteguliwa ambako imebainika kwamba msichana wa tatu, Melvis Mbaya, ambaye amekuwa nao mara kwa mara si ndugu yao halisi katika kuzaliwa.

Uamuzi huo ulifikiwa Aprili mwaka huu baada ya familia hizo kuomba msaada wa vipimo vya DNA ambako taasisi ya Lancet Kenya ikajitolea kufanya kazi hiyo kwa gharama nafuu.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, sehemu 12 kati ya sehemu 23 zinazotumika katika tathmini hiyo ya Melvis Mbaya zilikosa kufanana.

“Sehemu tatu tu zikikosa kuonyesha mfanano katika uchunguzi wa aina hii, inafafanuliwa kwamba matokeo ni hasi,” ilisema sehemu ya matokeo hayo ya uchunguzi wa DNA.

Hata hivyo, matokeo hayo yalionyesha Melvis Mbaya ana chembechembe sawa kabisa na za Angeline Omina na Wilson Lutah Maruti ikimaanisha kwamba huyo ni mtoto wa familia nyingine ya ndugu hao.

Wasichana hao ambao kwa sasa ni watahiniwa wa kidato cha nne, wamekuwa wakielezea kuwa tangu wakutane wamejenga urafiki wa karibu ambao ulionekana kuzidi hata undugu.