DPP asubiriwa kesi ya ‘Mpemba wa Magufuli’

Thursday April 18 2019

 

By Pamela Chilongola, Mwznanchi [email protected]

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi inayomkabili Yusuf Ali maarufu ‘Mpemba wa Magufuli' na wenzake watano umeeleza kuwa unasubiri kusainiwa kwa nyaraka zitakazowezesha kusikiliza shauri hilo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Yusuf na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne, likiwamo la kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6 milioni.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi amedai leo Alhamisi Aprili 18,2019 mbele ya Mahakama hiyo kuwa upelelezi umekamilika na kinachosubiliwa ni Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kusaini nyaraka zitakazowezesha kusikilizwa kwa kesi hiyo.

"DPP alikuwa hayupo sasa amerudi ndani ya siku saba atakuwa amesaini hivyo tunategemea wiki hii kuzipata,” ameeleza  Nchimbi.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Thomas Simba amesema anatarajia siku shauri hilo litakapofikishwa mahakamani hapo upande wa mashtaka utakuwa tayari.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 25 itakapotajwa tena na watuhumiwa wamerudishwa ndani.

Advertisement

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Charles Mrutu, mkazi wa Mlimba, Morogoro, Benedict Kungwa, mkazi wa Mbagala Chamazi, Jumanne Chima, mkazi wa Mbezi, Ahmed Nyagongo, dereva na Pius Kulagwa.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara, walijihusisha na mtandao wa ujangili kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola za Marekani 180,000 sawa na Sh 392.8 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

Advertisement