MADAI: DPP awatuhumu wabunge kwa rushwa, Spika ajibu

Monday May 27 2019Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga

Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Biswalo Mganga amesema baadhi ya wabunge wanapenyezewa rushwa na watu wanaokabiliwa na mashtaka au tuhuma mbalimbali za makosa ya jinai, ili wamshinikize katika utendaji wake.

DPP Mganga ameibua tuhuma hizo wakati akijibu tuhuma zilizotolewa na wabunge wawili wa upinzani, akiwamo Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), kwamba amekuwa akiwabambikizia watu kesi za utakatishaji fedha na kukubaliana nao walipe faini, kama chanzo cha kuongeza mapato ya Serikali.

Zitto, alipoulizwa jana na Mwananchi kuhusiana na kauli hiyo ya DPP, alisema kupitia ujumbe mfupi wa maandishi, “yeye ni DPP halafu anatoa hukumu?”

Kuhusu madai hayo ya DPP, Spika wa Bunge Job Ndugai alisema, “kama DPP kasema, ni jambo ambalo lazima tulifanyie kazi. Hatuwezi kudharau tukaanza kujikosha kusema hilo halipo au vipi.”

Hata hivyo, alisema bado hajapokea tuhuma hizo rasmi mezani kwake. “Ni jambo ambalo tutaliangalia kwa umakini maana vinginevyo, Bunge letu lisije kutumika vibaya. Hatulichukulii kwa urahisi,” alisema Ndugai.

Alipoulizwa ni umakini gani utakaotumika kufuatilia jambo hilo alisema, “sasa tukitaja mbinu tena si itakuwa tabu, tutaliangalia na tunalipokea kwa mikono miwili kwa kulishughulikia.”

Advertisement

Aprili 13, wakichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Tamisemi na Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Umma na Utawala Bora), Zitto alihoji DPP anatumia sheria ipi kujadiliana na washtakiwa ili kuwapunguzia au kufuta adhabu na kulipa faini akidai kuwa hakuna sheria wala kanuni ya aina hiyo. Pia alihoji mahali zinapokwenda fedha hizo za faini na anayezikagua.

DPP Mganga alisema yeye si mwanasiasa na hawezi kufanya kazi kwa kufuata siasa, sheria lakini anafahamu kuna rushwa ambayo inazunguka bungeni ili kumshinikiza katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Kama wanasema ninawalazimisha, na mahakamani nako ninawalazimisha?” alihoji.

Alisema kinachofanyika siku zote, washtakiwa wenyewe ndiyo huwa wanamweleza DPP kuwa wako tayari kukiri makosa yao na hawataki wapoteze fedha za Serikali kufanya upelelezi.

Alisema, “wanaandika barua na kama kuna mtu anataka ushahidi nitamuonyesha, ninachokifanya ni kuipatia Mahakama mamlaka yake kwa kuwaeleza waende wakakiri mahakamani.

“Sasa hapo nimewalazimisha? Nyie (waandishi) mnakuwepo mahakamani washtakiwa wanaposomewa mashtaka na wanavyojibu. Sasa DPP anawalazimisha kutokea wapi.

“Wewe unakuja umeniandikia, DPP mimi nakiri makosa yangu, acheni kupeleleza kesi, mimi nataka nikakiri mahakamani. Sasa nitakuwa DPP mpumbavu kuliko ma- DPP wote duniani, mtu anasema mimi nakiri makosa yangu halafu nasema ngoja tuendelee na upelelezi.”

Alisema kuna rushwa anaifahamu iliyokuwa inazunguka hadi ikaingia bungeni kuhusiana na kesi moja ya uhujumu uchumi na wabunge wakataka kumshinikiza, lakini akawaambia atafanya kazi kwa mujibu wa sheria na si kwa shinikizo.

Kuhusu madai kwamba hakuna sheria ya kujadiliana na washtakiwa, DPP alisema hoja hiyo inatokana na ama wanasiasa hao kutokuwa na uzoefu wa masula ya kisheria na utendaji kazi wa Mahakama au wanasahau.

“Ndio maana nikasema wawaulize wanasheria wazoefu. Ni mara ngapi watu wameenda mahakamani wanakiri makosa yao, kasome (CPA), Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka ya Jinai inasemaje,” alisema DPP Mganga.

Alihoji ni mara ngapi mtu anashtakiwa kwa kosa la kuua kwa kukusudia, lakini baadaye anakubali kosa dogo la kuua bila kukusudia na linabadilishwa kutoka kuua na kuwa kuua bila kukusudia.

“Hiyo sheria iko wapi?”, alihoji DPP Mganga na kufafanua kuwa desturi za Mahakama ni sehemu ya sheria.

Advertisement