VIDEO: Dakika tano za utambulisho wa Pierre Konki Liquid bungeni, wabunge wafunguka ujio wake

Mama Salma Kikwete upo juu, na wewe Pierre upo juu, hayo ndio maneno waliyokuwa wakiambiana na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Salma Kikwete na Peter Moller maarufu Pierre Konki Liquid walipokutana katika viwanja vya Bunge, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kualikwa bungeni kwa Peter Mollel maarufu Konki Liquid au Pierre, mwanaume aliyeishika mitandao ya kijamii wakati huu kumekuja ikiwa ni siku moja tu tangu Bunge kueleza uamuzi wake wa kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad. Ujio wake umepokewa kwa hisia tofauti na wabunge.


Dodoma. Wakati uamuzi wa Bunge kutofanya kazi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ukitikisa kila kona nchini Tanzania, Peter Mollel aliyejizolea umaarufu baada ya video iliyomuonyesha akisema “mama nakufa” leo Jumatano Aprili 3, 2019 ni miongoni mwa wageni walioalikwa bungeni jijini Dodoma.

Pierre aliyeshika mitandao ya kijamii wakati huu ambaye utambulisho wake zaidi ni maneno yake ya Konki Liquid, Pierre, Mama nakufa, Chii amealikwa kutembelea bungeni leo  huku Spika wa Bunge, Job Ndugai akisema “simjui mtu huyu” na kuwafanya wabunge kuangua vicheko.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na Mwananchi na kuulizwa kuhusu ujio wa Pierre na joto lililopo bungeni kwa sasa kutokana na uamuzi wa Bunge kutofanya kazi na CAG, wametoa maoni tofauti huku mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Ether Matiko akisema ulitumika muda mrefu kumtambulisha.

Ndugai wakati akitambulisha wageni mbalimbali waliofika bungeni leo Jumatano, Aprili 4 wakiwemo maspika wa nchi mbalimbali Ndugai amesema, “naomba wabunge tukae tusikilizane leo tuna wageni maarufu katika jukwaa la Spika.”

Baada ya kuwatambulisha wageni hao Ndugai amesema, “Nadhani wageni wameisha,” kauli ambayo iliwaibua wabunge na kupaza sauti wakisema bado hawajaisha, baadhi kutaja jina la Pierre.

“Yupo mgeni mmoja ambaye mimi simfahamu naomba nimpe heshima Mariam Ditopile (mbunge Viti maalum CCM) atumie dakika moja kumtambulisha mgeni huyu (Pierre), simfahamu,” amesema Ndugai.

Akitambulisha Pierre, Mariam amesema, “Mimi ni mbunge wa vijana, mgeni wetu wa mwisho kutambulishwa ni Pierre Liquid, huyu ni Mtanzania  mzalendo, mjasiriamali wa fenicha anayepatikana Changombe.”

“Ila baada ya kazi ni mpenda burudani na ana kijiwe chake kinaitwa Liquid ndio maana jina lake ni Liquid. Ila hivi karibuni ametoka kupata umaarufu wa hali ya juu ndani na nje ya nchi kutokana na sanaa ya vichekesho.”

Amesema umaarufu wa Pierre unatokana na sanaa ya vichekesho na kauli zake hufurahisha watu na kuwafanya wapunguze msongo wa mawazo.

“Mzee Majuto (marehemu) tunamuenzi kutokana na kipaji cha vichekesho na Liquid alileta hamasa Taifa Stars ikashinda bao 3, nimalize tu kwa kusema Mungu akitaka kukupa hakuandikii barua,” amesema Mariam na kuwafanya wabunge kushangilia kwa mtindo wa kipiga meza.

Baada ya utambulisho huo Ndugai amesema, “Timu yetu ya Taifa itashiriki michuano ya Afrika huko Misri. Pierre karibu sana bungeni, Magufuli utabaki kuwa juu, utabaki kileleni. Pierre wabunge hawajakuona uko wapi Pierre karibu sana mjengoni. Karibu sana Konki Fire.”

 

Walichokisema wabunge

Akizungumzia ujuo wa Pierre bungeni mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Bulaya amesema, “kuja kwake bungeni na kupewa muda ule wote anatambulishwa wakati kuna maswali ya nyongeza na watu walinyimwa (kuuliza) kwa sababu muda umekweisha.”

“Sikatai Konki ni Mtanzania na amehamasisha Taifa Stars na kuburudisha Watanzania, ila kutumia muda wa Bunge wa dakika tano kumtambulisha Konki wakati huo huo wamekataa  kutoa maswali ya wabunge ambao wapo hapa kuwakilisha wananchi.”

Ameongeza, “Leo Bunge lipo kwa ajili ya maswali na majibu na linaahirishwa, ila unampa muda mtu dakika tano kumtambulisha Piere, natambua mchango wake lakini hatukupaswa kupoteza muda wa Bunge.”

Mbunge wa Manonga (CCM), Seif Gulamali amesema “unajua hili ni Bunge la Watanzania, wananchi wote wana haki kuja kujifunza. Ujio wa Pierre au mzee wa Liquid si kwamba umewafurahisha wabunge, hata Watanzania wengine.”

“Pierre amehamasisha mambo mbalimbali hasa ushindi wa Taifa Stars, pamoja na kufurahisha naye anapata muda wa kujivunia matunda ya nchi yake.”

Kabla ya kuingia katika ukumbi wa chombo hicho cha Dola, Pierre alinyoosha mikono juu kama mtu anayemshukuru Mungu, akiwa ameongozana na watu wengine watatu.

Wakati akikaguliwa mlangoni, Mwananchi lilishuhudia akipiga picha na baadhi ya watu, kisha kuongozwa kwenda ukumbini.

“Naona leo amealikwa Pierre Liquid,” amesema mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete wakati akiuliza swali la nyongeza bungeni.