Dakika za mwisho joto la Ndugai, CAG

Muktasari:

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu  Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad  amesema ana nia ya kuitikia wito wa Spika Job Ndugai kwa sababu ofisi yake haiwezi  kufikia ufanisi unaohitajika katika utendaji wake kama ripoti zake hazifanyiwi kazi ya kuridhisha na Bunge


Dar es Salaam. Hatimaye joto la siku 13 lililoibuliwa na Spika Job Ndugai baada ya kumtaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad kufika mbele ya Kamati ya Bunge kuelezea kauli yake kuhusu “udhaifu wa Bunge”, zimetimia leo.

Kama alivyoahidi, Profesa Assad anatarajiwa kuitikia wito wa Spika alioutoa Januari 7 wa kumtaka afike mbele ya Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge na ameshaeleza kuwa neno “udhaifu” lililoibua mjadala, ni la kawaida katika lugha za kihasibu.

CAG Assad aliyeteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, Desemba Mosi mwaka 2014 ameitwa mbele ya kamati hiyo kujieleza kuhusu kauli aliyoitoa wakati alipokuwa akihojiwa na kituo cha televisheni cha idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa (UN) akiwa New York, Marekani alikokuwa akihudhuria mkutano.

Alitumia neno “udhaifu” wa Bunge alipokuwa akieleza sababu za kutofanyiwa kazi kwa ripoti zake ambazo zimekuwa zikibainisha ufisadi.

Akiwa na mwanasheria wake iwapo ataona inafaa, CAG atafika mbele ya kamati hiyo inayongozwa na mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Emmanuel Mwakasaka na ambayo ina wajumbe 17 kutoka vyama vya CCM, Chadema na CUF ambao wote huhudhuria.

Kwa kawaida, mtuhumiwa, ambaye huchukuliwa kama shahidi, hutakiwa kukaa kiti kinachotazamana na mwenyekiti wa kamati. Na huruhusiwa kuingia na mwanasheria wake au mtu mwingine anayeona anafaa, lakini hataruhusiwa kujibu neno lolote au kufafanua isipokuwa kushauriana na mtuhumiwa.

Na hata kama ataulizwa swali na mjumbe wa kamati hiyo, CAG atalazimika kujibu kwa kumueleza mwenyekiti na si muuliza swali.

CAG atayajua hayo yote wakati mwenyekiti atakapokuwa akifungua shauri na kumuelekeza jinsi kikao hicho kinavyoendeshwa na kumsomea tuhuma hizo kwa mujibu wa barua ya wito iliyotumwa na ofisi ya Bunge.

Baada ya mahojiano, CAG ataruhusiwa kwenda nje ya ukumbi na kutakiwa kusubiri kamati ijadili hoja zake na mwenendo wa mahojiano ili kama kuna haja ya kufafanua aitwe tena.

Baadaye ataitwa kuelezwa kuwa uamuzi wa shauri lake utafuata. Kamati hiyo itatakiwa kumrudishia Spika ripoti hiyo na mapendekezo ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa. Spika atakuwa na hiari ya kulisomea Bunge ripoti hiyo, au wabunge wanaweza kupendekeza adhabu baada ya kusomewa.

Hatua hizo pekee zaweza kuwa suluba tosha kwa mtendaji huyo mkuu wa Ofisi ya Hesabu za Serikali, ambaye amekuwa akitoa ripoti mbalimbali zinazoonyesha kutofuatiliwa kwa mapendekezo ambayo yanaonyesha udhaifu katika usimamizi wa fedha wa mashirika ya umma au Serikali.

Wakati hayo yakiendelea, Spika Ndugai amesitisha kufanya kazi na ofisi ya CAG na kuwatawanya wajumbe wa kamati mbili; ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuongeza nguvu kwenye kamati nyingine wakati huu ambao zitakuwa hazina majukumu.

PAC na LAAC zinazoongozwa na wenyeviti kutoka vyama vya upinzani, ndizo zimekuwa zikifanyia kazi ripoti za CAG na ratiba ya awali ya Bunge ilionyesha kamati hizo zingekuwa zikijadili ripoti ya sasa.

Hata hivyo, Januari 17, Profesa Assad aliita waandishi wa habari na kueleza nia yake ya kwenda mbele ya Kamati ya Maadili, akieleza kusikitishwa na jinsi kauli yake ilivyozua mjadala na kutia doa uhusiano baina ya ofisi yake na Bunge.

Awali, akiwa Marekani, akijibu swali la mwandishi wa televisheni ya UN, Anord Kayanda kuhusu kutoshughulikiwa ipasavyo kwa ripoti zake zinazoonyesha ufisadi, Profesa Assad alisema: “Kama tunatoa ripoti na kuna ubadhirifu na hatua hazichukuliwi huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa lisimamie na kuhakikisha kwamba pale kwenye matatizo hatua zinachukuliwa. Sasa sisi kazi yetu ni kutoa ripoti tu,” alisema CAG.

Lakini katika mkutano wake na waandishi wa habari wiki iliyopita, Profesa Assad alionyesha kutaka busara zitawale suala hilo.

“Tunachoshauri sisi ni kwamba uungwana utawale katika mawasiliano yetu,” alisema Profesa Assad.

Alisema kauli yake haikulenga kulidhalilisha Bunge na kwamba neno udhaifu ni la kawaida hasa kwenye kada hiyo ya ukaguzi na amekuwa akilitumia hata katika ripoti zake.

Kauli hiyo ya CAG kuwa Bunge ni dhaifu haikumpendeza Spika Ndugai, ambaye siku chache baadaye alimtaka kufika mbele ya kamati hiyo kwa hiari vinginevyo atapelekwa kwa pingu.

“Pamoja na kwamba analindwa na Katiba namshauri sana CAG ajitathmini upya. Hatutavumilia hata dakika moja kudharauliwa na mtu yeyote na tutakasirika zaidi dharau hizo ukizifanyia nje ya nchi,” alisema Spika Ndugai.

Spika huyo alitoa wito pia kwa mbunge wa Kawe, Halima Mdee baada ya kusema anaunga mkono kauli ya CAG.

Kwenye sakata hilo wapo viongozi mbalimbali waliomuunga mkono Spika akiwamo Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum ambaye alimpongeza Spika kuwa ni kiongozi ambaye akimuita mtu lazima aende.

Wataalamu wa masuala ya sheria walidai kuwa wito huo unakiuka matakwa ya sheria na kwamba kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa CAG kama anavyolindwa na Katiba chini ya ibara 143(6).

Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume naye alisema Spika hana mamlaka ya kumuita CAG.

“Kulidhalilisha si kulikosoa. Huwezi kumwambia mtu ni dhaifu halafu ukasema hiyo ni kudhalilisha na kama kalidhalilisha Bunge nje, mkondo wa sheria ya jinai unachukua nafasi yake, si Bunge,” alisema Karume.

Katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif alimpongeza CAG kwa kuchagua kuwa muungwana katika kulishughulikia suala hilo.

Mahakamani

Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe na Rais wa TLS, Fatma Karume walitinga mahakamani kufungua kesi ya kikatiba ya kupinga kitendo cha kuhojiwa CAG.

Hata hivyo kesi yao ilishindikana kusajiliwa kwa siku tano mfululizo baada ya kufikishwa mahakama Kuu Januari 14 na mahakama kusema kuwa ina kasoro.

Mahakama hiyo ilisema kesi hiyo ina kasoro ikiwamo kutoambatanisha hati za viapo pamoja na wito wa Spika.

Maoni ya wabunge

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF) aliliambia Mwananchi kuwa anaamini suala hilo litamalizika vizuri kwa kuwa taasisi hizo zinatakiwa kusimamia maslahi ya wananchi. “Mimi naamini uhusiano utaendelea kuwepo kwa sababu CAG mwenyewe amesema mahusiano ya Bunge na ofisi yake ni muhimu, akihojiwa ataeleza kile ambacho nafsi yake inamtuma...watasuluhisha,” alisema Sakaya.

Wabunge wa CCM nao walimpongeza Profesa Assad kuitikia wito wa kamati licha ya kuwepo kwa propaganda wanazodai zinaenezwa kwenye vyombo vya habari na mitandao ya jamii kwa lengo la kupotosha suala hilo.

Akizungumza jana kwa niaba ya wabunge wenzake, mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda alisema hatua ya CAG kukubali kuhojiwa na Bunge ni ya kiungwana.