MAUAJI YA MWANAFUNZI WA SCOLASTICA: Daktari: Nilitumia meno kukadiria umri wa marehemu

Mshitakiwa wa kesi ya mauwaji ya mwanafunzi Huphrey Makundi wa Shule ya Sekondari ya Scolasti ,Edward Shayo akelekea katika chumba cha mahakama ya Hakimu Mkazi moshi Mjini kwaajiri ya kusomewa mashitaka yanayo mkabili.Picha na Mpiga picha wetu.

Muktasari:

Juzi, Jackson Makundi, baba mzazi wa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Scolastica, Humphrey Makundi (16) ali-ieleza Mahakama namna alivy-outambua mwili wa mwanaye baada ya kufukuliwa.Shahidi huyo alidai pia kuwa mmoja wa wanafunzi ali-yekuwa akisoma na mwanaye alimsisitizia afuatilie tetesi kuwa kuna mwanafunzi ali-pigwa na kuumizwa nyuma ya ukuta wa shule.Mwanaye aliyekuwa akisoma kidato cha pili katika shule hiyo, alitoweka shuleni hapo Novemba 6, 2017 na baadaye mwili wake ulibainika kuzikwa na Manispaa ya Moshi kwa madai ya kutotambuliwa. Akitoa ushahidi wake kama shahidi wa tatu wa upande wa mashtaka, Makundi alidai Novemba 17, 2017 walifanikiwa kupata amri ya Mahakama ya kuufukua mwili huo ukiwa umekaa kaburini kwa siku sita.

Moshi. Shahidi wa nne, Dk Samwel Mwita, ameieleza Mahakama Kuu namna alivyotumia mfumo wa meno kukadiria umri wa mwanafunzi wa shule ya Scolastica, Humphrey Makundi aliyeuawa Novemba 2017.

Dk Mwita aliyasema hayo juzi jioni wakati akitoa ushahidi katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mwanafunzi huyo inayosikilizwa na Jaji Firmin Matogolo wa Mahakama Kuu.

Kesi hiyo inayowakabili washtakiwa watatu akiwemo mmiliki wa shule hiyo Edward Shayo, mwalimu wa nidhamu Laban Nabiswa na mlinzi Hamis Chacha, juzi ilisikilizwa hadi saa 1:20 usiku.

Mwanafunzi huyo alitoweka shuleni Novemba 6,2017 na baadaye ilibainika ameuawa na watu wasiojulikana baada ya mwili wa mtu aliyedaiwa ni mtu mzima mwenye ndevu kufukuliwa kwa amri ya Mahakama.

Mwili wa mtoto huo uliokotwa Novemba 10 katika mto Ghona ikiwa ni takriban mita 300 kutoka shuleni na polisi waliouchukua waliupeleka Hospitali ya Mawenzi na kuzikwa kwa madai kutotambuliwa.

Dk Mwita ambaye ni daktari wa kinywa na meno katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC aliieleza Mahakama kuwa Novemba 19, 2017 ulipelekwa mwili ambao ulikuwa umeharibika ili ufanyiwe uchunguzi.

Shahidi huyo aliongozwa kutoa ushahidi wake na wakili mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavulla ambaye ni miongoni mwa jopo la mawakili wanne wa mashtaka walioongozwa na Joseph Pande.

Alidai kuwa kulingana na taaluma yake, alihitajika kufanya uchunguzi wa meno na taya ili kukadiria umri wa marehemu ambapo alijiridhisha kuwa ulikuwa kati ya miaka 14 na 17.

“Viungo ambavyo vinaweza kukadiria umri ni meno yake na katika ule uchunguzi mwili wa marehemu haukuwa na meno (magego) ya mwisho yalikuwa bado kwenye mfupa,” alidai.

Daktari huyo alidai umri wa wa chini wa meno hayo kutoka ni miaka 18, hivyo kwa kuuchunguza mwili wa marehemu, gego la pili lilikuwa limeshaota hivyo aliukadiria kuwa na umri huo.

“Kwa kutazama taya zote mbili, nilijiridhisha kuwa marehemu alikuwa na umri wa kati ya miaka 14 na 17 na kabla ya mwili ule kufanyiwa uchunguzi ulikuwa haujafahamika umri wake,” alidai.

Kwa upande wake, shahidi wa tano wa mashtaka, Anastazia Januari ambaye ni muuguzi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi, aliieleza Mahakama hiyo namna mwili huo ulivyofikishwa hapo.

Shahidi huyo aliiambia Mahakama kuwa Novemba 10, 2017 kati ya saa 2 na saa 3 usiku, alipokea mwili wa mtu asiyefahamika kutokea Himo na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.

Alidai muda huo alifika askari aliyejitambulisha kwa jina la Inspekta Juma akiwa na gari la polisi ambalo lilikuwa limebeba mwili huo kwa lengo la kuuhifadhi katika chumba cha kuhifadhia maiti.

“Kwa maelezo ya askari yule, mwili ule haukutambulika ni wa nani, lakini jinsia aliniambia ni ya kiume na kama ilivyo taratibu nilichukua taarifa zake na baadaye nikamwita mlinzi,” alidai.

Kwa mujibu wa shahidi huyo, mlinzi huyo alichukua funguo na kwenda kufungua chumba cha kuhifadhia maiti na kuuhifadhi, lakini akadai yeye hakwenda kuhakiki mwili, bali aliona ukishushwa.

Akitoa ushahidi wake jana, shahidi wa sita, Koplo Shaban Omary alidai Novemba 20, 2017, alikabidhiwa sampuli za vinasaba (DNA) kwa ajili ya kuzipeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam.

Alidai kuwa sampuli hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kuchunguza uwiano wa DNA kati ya mwili wa marehemu uliookotwa na wazazi ambao ni baba yake, Jackson Makundi na Joyce Jackson ambaye ni mama.

Sampuli hizo ni pamoja na kipande cha mfupa wa paja na meno mawili ya marehemu, damu na mate ya wazazi wa mtoto aliyedhaniwa mwili ulikuwa wake.

Shahidi huyo alidai kuwa alisafiri kwa ndege hadi jijini Dar es Salam na alipoka ofisini kwa Mkurugenzi wa Upelelezi nchini (DCI), alikabidhiwa jokofu kwa ajili ya kuhifadhia sampuli hizo kwa kuwa baadhi zinaathiriwa na joto la nje.

Mbali na kupeleka sampuli hizo, lakini shahidi huyo alidai kuwa Januari 30, 2018 alikabidhiwa simu saba ili kuzipeleka kitengo cha makosa ya mtandao katika ofisi ya DCI jijini Dar es Salaam.

Imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba na Janet Joseph