Daladala Mbeya shwari, Moshi bado

Muktasari:

  • Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya alisema ni ndoto kuondoa Bajaj katikati ya mji lakini wamiliki wanatakiwa walipe ushuru.

Moshi/Mbeya. Wakati wakazi wa mji wa Moshi wakilazimika kutafuta usafiri mbadala kutokana na kuendelea kwa mgomo wa daladala, hali ni shwari mjini Mbeya ambako pande tatu zilikutana na kufikia muafaka uliorejesha huduma hiyo jana.

Mjini Moshi, madereva wa mabasi ya daladala waligoma kutoa huduma wakidai kuwa waendesha pikipili za magurudumu matatu, maarufu kwa jina la Bajaj, wanatoa huduma kama hiyo lakini hawalipi ushuru Sh1,000 wa maegesho.

Hali kama hiyo ilijitokeza Mbeya ambako madereva hao walikuwa wakilalamikia Bajaj kufanya kazi kibiashara kwenye barabara kuu na hivyo kuanzisha mgomo uliosababisha nauli kupanda kutoka Sh500 hadi Sh1,000 kwa Bajaj na Sh3,000 hadi Sh5,000 kwa bodaboda.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wananchi wa mji wa Moshi na vitongoji vyake walisema hawaoni tena sababu ya kutumia daladala wakati Bajaj zipo za kutosha.

“Wao waendelee kugoma tu, sisi ambao tupo hapa mjini hatupati shida ya usafiri, bajaji zipo za kutosha na zinatufikisha hadi nyumbani tena kwa wakati,” alisema mkazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Jesca Gasper.

Mkazi mwingine anayeishi Majengo, Amate Joseph alisema wanachokifanya madereva hao wa daladala ni kujipotezea tu muda kwa sababu Bajaj zinafanya kazi kama kawaida.

“Wanapoteza muda kuigomea manispaa kulipa ushuru. Huku barabarani kila mtu amekuja kutafuta riziki yake,” alisema Joseph.

Lakini wapo wanaohangaika kutokana na mgomo huo wa siku saba, kama wakazi wa kata ya Msaranga ambao wanalazimika kutembea kilomita mbili kufuata Bajaj.

Jenifa Thomas, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Majengo, alisema: “Mgomo unatuathiri sana sisi wanafunzi ambao usafiri wetu mara nyingi ni daladala.”

Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya alisema ni ndoto kuondoa Bajaj katikati ya mji lakini wamiliki wanatakiwa walipe ushuru.

Mjini Mbeya, madereva wa daladala, Bajaj na Sumatra walikutana juzi na kufikia muafaka.

Ofisa mfawidhi wa Sumatra, Denis Daudi alisema kilichokuwa kinasubiriwa ni tamko la Serikali ambalo mchana huu (jana) limetolewa stendi ya Kabwe mbele ya wahusika hivyo huduma ya usafiri imesharejea.

Mwenyekiti wa nidhamu wa Bajaj, Steven Matengo alisema watahakikisha wanasimamia na kuondoa Bajaj zinazofanya biashara kwenye barabara kuu kwa kuwa ndicho kimekuwa chanzo cha mivutano ya mara kwa mara kati yao na madereva.

Rachel Odongo, mkazi wa Mbata, alifurahishwa na kurejea kwa huduma hiyo, akisema sasa shughuli zitaendelea kama ilivyokuwa awali.